79. An-Naazi'aat
1Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Malaika ambao huzing’oa roho za makafiri mng’oo mkali
2Na kwa Malaika ambao huzitukua roho za Waumini kwa uchangamfu na upole
3Na kwa Malaika wanaoogelea katika kushuka kwao kutoka mbinguni na kupaa kwao kwenda mbinguni
4Na kwa Mlaika ambao wanakimbilia kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu
5Na kwa Malaika wanaopitisha amri za Mola wao katika mambo ya ulimwengu waliowakilishwa kuyafanya na kuyasimamia, - Wala haifai kwa kiumbe kukiapia chochote kile, bali yapasa kiapo chake kiwe ni kwa jina la Mola wake Muumba au sifa Zake. Na lau ataapa kwa asiye Muumba wake, basi huyo amekuwa mshirikina - Watafufuliwa viumbe bila shaka na watahesabiwa
6Siku ambayo ardhi itatetemeka kwa mvuvuo wa kwanza
7mvuvio wa kufisha, ukifuatiwa na mvuvio mwingine wa kuhuisha
8Nyoyo za makafiri, Siku hiyo, zitakuwa na papatiko kwa kicho kikubwa
9Macho ya makafiri hao yatakuwa madhalilifu kwa kitisho watakachokiona
10Wanasema hawa wakanushao kufufuliwa
11«Je, tutarudishwa baada ya kufa kwetu kwenye yale tuliyokuwa nayo katika ardhi? Je, tutarudishwa na hali tushakuwa mifupa iliochakaa?»
12Wakasema: «Kurejea kwetu huko kutakuwa kutupu kusikokuwa kweli.’
13Hakika tukio hilo litakuwa kwa mvivio mmoja tu
14Wakitahamaki wao wako hai juu ya ardhi baada ya kuwa walikuwa ndani yake
15Je imekujilia, ewe Mtume, habari ya Mūsā
16Pindi Mola wake Alipomwita katika bonde lililotakaswa na kubarikiwa, la Ṭuwā. Akamwambia
17«Enda kwa Firauni. Hakika yeye amekiuka mno katika kuasi
18Ukamwambie, ‘Je, unapendelea kuitakasa nafsi yako na upungufu na kuipamba na imani
19Na nikuelekeze njia ya kumtii Mola wako, upate kumcha na kumuogopa?’»
20Mūsā alimuonyesha Firauni alama kubwa: fimbo na mkono
21Hapo Firauni alimkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu , naye ni Mtume Mūsā, amani imshukie, na alimuasi Mola wake Aliyetukuka
22Kisha alikengeuka hali ya kuipa mgongo Imani na kufanya bidii katika kumpinga Mūsā
23Hapo aliwakusanya raia wa utawala wake na akawaita kwa
24kuwaambia,»Mimi ndiye mola wenu ambaye hakuna mola mwengine aliye juu yake.»
25Hapo Mwenyezi Mungu Alimtesa kwa adhabu ya duniani na ya Akhera
26Na Akaifanya adhabu hiyo iwe ni mazingatio na ni onyo kwa watu mfano wake kati ya wale waasi. Hakika Firauni na kile kilichompata cha adhabu ni mawaidha kwa mwenye kuwaidhika na kutishika
27Je, kufufuliwa kwenu, enyi watu, baada ya kufa ni kugumu zaidi, katika vipimo vyenu, au ni kuumbwa kwa mbingu
28Amezipanga juu yenu kama jengo. Na Ameinua sakafu yake angani, haina tofauti wala nyufa
29Na Ameutia giza usiku wake kwa kutwa kwa jua lake. Na Ameweka wazi mchana wake kwa kuchomoza kwake
30Na ardhi baada ya kuumba mbingu Ameitandaza. Na Ameweka humo manufaa yake
31Na Ametumbua humo chemchemu za maji. Na Ameotesha humo mimea inayolishwa
32Na Ameyakita humo majabali yakiwa ni vigingi vyake. Ameumba, Aliyetakasika na kila upungufu
33neema zote hizi zikiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu. (Hakika kurudisha kuumbwa kwenu, Siku ya Kiyama, ni sahali kwa Mwenyezi Mungu kushinda kuumba viumbe hivyo vyingine. Na vyote hivyo, kwa Mwenyezi Mungu, ni rahisi na ni vipesi)
34Pindi kitakapokuja Kiyama Kikubwa na balaa nzito, nao ni Mvuvio wa pili. Kipindi hicho zitaoneshwa kwa binadamu vitendo vyake vyote, za kheri na za shari
35Hapo atazikumbuka na kuzitambua
36Na utaoneshwa Moto wa Jahanamu kwa kila aonaye, uwe waonekana waziwazi
37Ama yule atakayekiuka amri ya Mwenyezi Mungu
38na akapendelea maisha ya ulimwenguni kuliko ya Akhera
39basi kwa kweli marejeo yake ni Motoni
40Na ama yule atakayeogopa kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu kuhesabiwa na akaikanya nafsi yake na matamanio mapotofu
41basi Peponi ndiko makazi yake
42Wanakuuliza washirikina, ewe Mtume, kwa madharau, kuhusu wakati wa kuanzia Kiyama unachowaonya
43Wewe huna kamwe ujuzi nacho
44Bali mambo ya ujuzi huo yarejeshwe kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye Sifa Tukufu
45Wewe linalokuhusu katika habari zake ni kumuonya nacho yule anayekiogopa
46Kama kwamba wao siku watakapouona Kiyama kimesimama, watakuwa hawakukaa katika maisha yao ya duniani, kwa vituko vya hiko Kiyama, isipokuwa ni kama kwamba wamkaa kati ya adhuhuri mpaka kutwa juwa, au ni kama kati ya kuchomoza jua mpaka nusu ya mchana
chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr
WEBREATH · 11:11
«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7
Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.
WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath