Uislamu
nyuma

70. Al-Ma'aarij

1Ameapiza mwenye kuapiza miongoni mwa washirikina, kujiapiza mwenyewe na kuwaapiza watu wake kuteremkiwa na adhabu

2nayo ni yenye kuwashukia bila shaka Siku ya Kiyama

3Hakuna mzuiaji yoyote wa kuizuia isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mwenye utukufu na haiba

4Malaika na Jibrili wanapanda kuenda Kwake, Aliyetukuka, kwa siku moja ambayo kadiri yake ni myaka elfu hamsini katika myaka ya duniani, nayo kwa aliyeamini ni kama muda wa Swala moja ya faradhi

5Basi vumilia, ewe Mtume, kule kufanya kwao shere na kutaka kwao wafikiwe na adhabu kwa haraka, uvumilivu usiokuwa na babaiko wala kumshtakia asiyekuwa Mwenyezi Mungu

6Kwa kweli makafiri wanaiona adhabu kuwa iko mbali na wanaona kuwa si yenye kutukia

7Na sisi tunaiona ni yenye kutukia kwa kipindi cha karibu bila shaka

8Siku ambayo mbingu itayayuka iwe ni kama rojo la mafuta

9na majabali yawe ni kama sufi iliyochanganywa na iliyoshanuliwa na kupeperushwa na upepo

10Wala mtu hatamuuliza jamaa yake wa karibu kuhusu jambo lake, kwani kila mmoja ameshughulishwa na nafsi yake

11Watawaona na watawajua, na hakuna yoyote atakayeweza kumnufaisha yoyote. Kafiri atatamani lau ajikomboa nafsi yake na adhabu ya Siku ya Kiyama kwa watoto wake

12mkewe, nduguye

13jamaa zake wanaomuhami na ambao anajinasibisha nao kwa ujamaa

14na kwa wote walio kwenye ardhi miongoni mwa binadamu na wengineo ili aokoke na adhabu ya Mwenyezi Mungu

15Mambo siyo kama vile unavyotamani yawe, ewe kafiri, ya kujikomboa

16Huo ni moto wa Jahanamu, moto wake unawaka na kuroroma, joto lake linatoa kwa nguvu ngozi ya kichwa na sehemu nyingine za mwili

17unamwita aliyeipa mgongo haki duniani na akaacha kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake

18na akakusanya mali na kuyaweka kwenye mahazina yake na asitekeleze amri ya Mwenyezi Mungu kwenye mali hayo

19Hakika binadamu ameumbwa akiwa na tabia ya babaiko na pupa

20Yakimpata makero na shida, anababaika sana na kufa moyo

21Na yakimpata mambo mazuri na ukunjufu wa maisha, huwa ni mwingi wa kuzuia na

22Isipokuwa wenye kusimamisha Swala

23wanaochunga kuitekeleza katika nyakati zake zote, hakuna shughuli yoyote inayowashughulisha nayo

24Na wale ambao katika mali yao kuna fungu maalumu alililowafaradhia Mwenyezi Mungu, nalo ni Zaka

25wanaozitoa kwa anayeomba msaada na kwa na kwa asiyeomba

26Na wale ambao wanaiamini Siku ya kuhesabiwa na kulipwa wakajiandaa nayo kwa matendo mema

27Na wale ambao wao wanaiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu

28kwani adhabu ya Mola wao haipaswi kwa yoyote kujiaminisha nayo

29Na wale ambao wao ni wenye kutunza tupu zao na kila alichokiharamishia Mwenyezi Mungu

30isipokuwa wake zao na vijakazi vyao, hakika wao kwa hao hawapatilizwi

31Basi mwenye kutaka kumaliza matamanio yake ya kimwili kwa wasiokuwa wake zake au vijakazi vyake, basi hao ndio wenye kukiuka mipaka ya halali kuingia kwenye haramu

32Na wale ambao wanazitunza amana za Mwenyezi Mungu na amana za waja, na wanatunza ahadi zao pamoja na Mwenyezi Munmgu, Aliyetukuka, na pamoja na waja

33Na wale ambao wanatekeleza ushahidi wao kwa ukweli bila kubadilisha au kuficha

34Na wale ambao wanatunza utekelezaji Swala wala hawaharibu chochote cha wajibu katika hiyo Swala

35Hao waliosifika kwa sifa hizo njema, ni wenye kutulia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe, ni wenye kukirimiwa humo kwa kila aina ya takrima

36Ni msukumo gani unaowasukuma makafiri watembee kwa haraka kuelekea upande wako, ewe Mtume, na huku wamenyosha shingo zao kwako, wamekukabili kwa macho yao

37wanajikusanya kuliani kwako na kushotoni kwako, wakiwa wamekaa kwa kupiga maduara na wamejigawa vikundi mbalimbali, wanazungumza na kuona ajabu

38Je ana tamaa kila mmoja miongoni mwa makafiri kuwa Mwenyezi Mungui Atamuingiza kwenye Pepo ya starehe ya daima? Mambo siyo kama vile wanavyotazamia. Wao hawataiingia hiyo Pepo kabisa

39Hakika sisi tumewaumba kwa kile wanachokijua cha maji matwevu kama wengineo, na vilevile hawakuamini. Basi vipi watapata heshima ya kuingia Pepo ya sterehe

40Sivyo hivyo. Najiapia Mimi Mwenyewe niliye Mola wa pande za kuchomoza na kutua jua, mwezi na sayari nyinginezo, kwa yanayopatikana humo miongoni mwa dalili waziwazi za kujulisha kufufuliwa

41kuwa Sisi tunaweza kuwaleta watu badala yao walio bora zaidi kuliko wao na watiifu zaidi wa Mwenyezi Mungu. Na hakuna yoyote atakayetushinda na kutuponyoka na kutuelemea iwapo tunataka kumrudisha uhai baada ya kufa

42Basi waache wavame kwenye ubatilifu wao na wacheze kwenye ulimwengu wao mpaka wakutane na Siku ya Kiyama ambayo wanaahidiwa kuwa wataadhibiwa

43Siku watakapotoka makaburini wakienda kwa haraka, kama wlivyokuwa duniani wakienda mbio na haraka kwa waungu wao wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu

44hali ya kuwa macho yao ni madhalilifu yanatazama chini, wamefinikwa na unyonge na utwevu. Hiyo ndiyo Siku waliyoahidiwa duniani na walikuwa wakiifanyia shere na kuikanusha

chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr

WEBREATH · 11:11

«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath