Uislamu
nyuma

56. Al-Waaqia

1Kitakaposimama Kiyama

2Hakutakuwa na yoyote mwenye kukanusha kusimama kwake

3Ni chenye kuwainamisha chini maadui wa Mwenyezi Mungu ndani ya Moto na ni chenye kuwainua juu Peponi wale wenye kumtegemea

4Itakapotikiswa ardhi mtikiso wa nguvu

5Na yakamumunyuliwa majabali mmumunyuo wa kina

6Yakawa vumbi lenye kuruka angani lililosukumwa na upepo

7Na mkawa, enyi viumbe, makundi matatu

8Kundi la watu wa upande wa kulia, wenye daraja kubwa. Ni kikubwa kilioje cheo chao

9Kuna na kundi la watu wa upande wa kushoto, wenye daraja duni. Ni mbaya iliyoje hali yao

10Na wale waliotangulia mbele kwenye kheri duniani ndio wenye kutangulia mbele kwenye daraja za juu huko Akhera

11Wao ndio walioletwa karibu kwa Mwenyezi Mungu

12Mola wao Atawatia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe

13Watayaingia watu wengi watu wa mwanzo wa ummah huu, na ummah wengineo wasiokuwa wao

14na wachache miongoni mwa watu mwisho wa ummah huu

15wakiwa juu ya vitanda vilivyofumwa kwa dhahabu

16na wakiwa katika hali ya kuvitegemea na huku wanaelekeana na kukutana

17Wanawazunguka wao kuwatumikia watumishi vijana wasiozeeka wala kufa

18wakiwa na vikombe, mabirika na gilasi kutoka kwenye chemchemi ya pombe yenye kupita ndani ya Pepo

19na hawaumwi na vichwa kutokana nayo wala hawarukwi na akili

20Na watawazunguka wao watumishi vijana na kila kitu wanachokichagua miongoni mwa matunda

21nyama ya ndege ambayo nafsi zao inavutika nayo

22Na watakuwa na wanawake wenye macho makubwa kama kwamba wao

23kwa usafi wao na uzuri wao, ni lulu iliyohifadhiwa ndani ya mashaza yake

24hali hayo yakiwa ni malipo yao kwa yale waliokuwa wakiyafanya duniani

25Hawatasikia humo Peponi ubatilifu wala yale ya kuwatia madhambini kuyasikia

26isipokuwa maneno yasiyokuwa na kasoro hizi na kusalimiana wao kwa wao

27Na watu wa upande wa kulia

28ni kikubwa kilioje cheo chao na malipo yao

29Watakuwa kwenye mikunazi isiyo na miba, na ndizi zilizopandana na kupangika

30kila ndizi juu ya nyingine, na vivuli vya daima visivyoondoka

31na maji yanayotembea yasiyokatika

32na matunda mengi

33yasiyomalizika wala kuwaishia wala hakuna kizuizi chochote kinachowazuia wao kuyafikia

34na matandiko yaliyoinuliwa juu ya vitanda

35Sisi tumewaumba wanawake wa watu wa Peponi umbile ambalo silo lile umbile lililokuwa duniani, umbile lililokamilika lisilokubali kutoweka

36na tumewafanya ni wanawali wenye kujipendekeza kwa waume zao

37hali ya kuwa ni marika na wao kimiaka

38Tumewaumbia wanawake hao watu wa upande wa kulia

39Nao ni kundi la watu wengi wa mwanzo

40na kundi la watu wengi wa mwisho

41Na watu wa upande wa kushoto, ni mbaya iliyoje hali yao na malipo yao

42Watakuwa kwenye upepo ulio moto utokanao na joto la Moto wa Jahanamu utakaozuia pumzi zao, na maji moto yanayochemka

43na kivuli cha moshi mweusi sana

44usio na mashukio baridi wala mandhari mazuri

45Kwani wao walikuwa duniani wakijistarehesha kwa vitu vya haramu wakijiepusha na yale ambayo Mitume walikuja nayo

46Na walikuwa wamesimama wima katika kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumshirikisha na kumuasi, na hawakuwa na nia ya kutubia kwa hayo

47Na walikuwa wakisema hali ya kukanusha Ufufuzi, «Je hivi sisi tutafufuliwa tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa iliyochakaa?» Maneno yao hayo yanaonesha kuwa wao walikuwa wakiliona jambo hili la kufufuliwa kuwa liko mbali na ukweli na wakilikanusha

48«Je tutafufuliwa sisi na hali baba zetu waliotangulia wamekuwa mchanga uliotapakaa kwenye ardhi?»

49Sema uwaambie, «Hakika wa mwanzo na wa mwisho miongoni mwa binadamu

50watakusanywa katika Siku iliyowekewa wakati maalumu, nayo ni Siku ya Kiyama

51«Kisha nyinyi, enyi mliopotea njia ya uongofu mnaokanusha onyo la Mwenyezi Mungu na agizo Lake

52ni wenye kula kutokana na mti wa zaqqūm

53nao ni katika miti mibaya zaidi, na ni wenye kujaza matumbo yenu kutokana nao kwa sababu ya ukali wa njaa

54na ni wenye kunywa juu yake maji yaliyo moto hadi ya mwisho, yasiyomaliza kiu

55Mtayanywa maji hayo kwa wingi kama vile ngamia wenye kiu wasioshiba maji kwa ugonjwa uliowapata.»

56Adhabu hii watakayoipata ndiyo zawadi Aliyowaandalia Siku ya Kiyama. Katika haya kuna kuwalaumu na kuwacheza shere

57Sisi tumewaumba, enyi watu, na hamkuwa kitu chochote. Basi si msadiki kuwa kuna kufufuliwa

58Mnayaonaje maji ya manii mnayoyatupa ndani ya vizazi vya wake zenu

59je nyinyi ndio mnaomuumba mwanadamu kutokana na hayo au ni sisi ndio wenye kuumba

60Sisi tumekadiria kifo kwenu

61na sisi si wenye kushindwa kubadilisha umbo lenu Siku ya Kiyama na kuwaumba kwa sifa na namna msizozijua

62Na hakika mlijua kuwa Mwenyezi Mungu Aliwaumba uumbaji wa kwanza na hamkuwa kitu chochote. Basi si mkumbuke uweza wa Mwenyezi Mungu wa kuwaumba mara nyingine

63Mnazionaje mbegu mnazozipanda

64Je ni nyinyi mnaoziotesha kutoka ardhini? Sisi ndio tuaozituliza na kuziotesha ardhini

65Lau tungalitaka tungaliifanya mimea inayotokana na mbegu hizo kuwa mapepe, haimkiniki kunufaika nayo kwa kula

66mkawa mnaona ajabu kwa kilichoshukia mimea yenu na mnasema, «Sisi tumepata hasara na ni wenye kuungulika

67Bali sisi tumekoseshwa riziki.»

68Mnayaonaje maji mnayokunywa ili mhuike kwayo

69Je ni nyinyi mliyoyateremsha kutoka kwenye mawingu hadi kwenye kituo cha ardhi au ni sisi tuliyoyateremsha ili kuwarehemu nyinyi

70Lau tungalitaka tungaliyafanya maji haya yawe na chumvi sana, ikiwa haiwezekani kunufaika nayo kwa kunywa wala kwa mimea. Basi si mumshukuru Mola wenu kwa kuteremsha maji tamu kwa kuwanufaisha nyinyi

71Mnaouonaje moto mnaouwasha

72Je ni nyinyi mlioufanya mti wake, unaozalisha moto kwa kukwaruzwa, upatikane au ni sisi tulioufanya upatikane

73Sisi tumeufanya moto wenu mnaouwasha ni ukumbusho kwenu wa Moto wa Jahanamu na pia ni manufaa kwa wasafiri

74Basi mtakase Mola wako, ewe Nabii, Aliye mtukufu Mwenye ukamilifu wa majina na sifa, Mwingi wa wema na kheri

75Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mapomoko ya nyota nyakati za kuzama kwake mbinguni

76Nacho ni kiapo kikubwa lau mnajua kadiri yake

77Hakika hii Qur’ani iliyoteremshiwa Muhammad ni Qur’ani yenye manufaa makubwa, yenye kheri nyingi na yenye elimu tele

78iliyo ndani ya Kitabu kilichohifadhiwa, kilichofichwa na macho ya viumbe, nacho ni Kitabu ambacho kiko mikononi mwa Malaika

79Hawaigusi Qur’ani isipokuwa malaika watukufu ambao Mwenyezi Mungu Amewasafisha na aibu na madhambi. Na pia hawaigusi isipokuwa watu waliojitohirisha na ushirikina na janaba na ukosefu wa udhu

80Na hii Qur’ani tukufu imeteremshwa kutoka kwa Mola wa viumbe vyote, kwani hiyo ndiyo haki isiyo na shaka ndani yake

81je hii Qur’ani, enyi washirikina, mnaikanusha

82Na je mnaifanya shukrani yenu kwa neema za Mola wenu ni kuwa nyinyi mnazikanusha na kukufuru? Hapa pana makaripio kwa anayedharau amri za Qur’ani na kutojali mwito wake

83Basi je mnaweza pindi roho ya mmoja wenu inapofika kwenye koo katika uchungu wa kifo

84na hali nyinyi mmehudhuria mnamtazama, kuizuia roho yake ndani ya mwili wake? Hamtaweza hilo

85Na sisi tuko karibu na yeye zaidi, kupitia Malaika wetu, kuliko nyinyi, lakini nyinyi hamuwaoni

86Na je mnaweza, iwapo nyinyi si wenye kuhesabiwa wala kulipwa kwa matendo yenu

87kuirudisha roho kwenye mwili, iwapo nyinyi ni wakweli? Hamtaweza kuirudisha

88Basi iwapo yule anayekufa ni kati ya watu wa upande wa kulia, atapata rehema kunjufu na furaha

89wakati wa kufa kwake, na kila kinachoifurahisha nafsi yake, Na atapata Pepo ya starehe huko Akhera

90Na iwapo yule anayekufa ni kati ya watu wa upande wa kulia

91ataambiwa, «Umesalimika na kuwa kwenye amani, kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu wa upande wa kulia.»

92Na iwapo yule anayekufa ni miongoni mwa wenye kukanusha kufufuliwa, waliopotoka na njia ya uongofu

93basi atapata makaribisho ya kinywaji cha moto wa Jahanamu kilichochemshwa, kilicho na joto hadi ya mwisho

94na atachomwa na Moto na aungulike na adhabu yake kali

95Hakika habari hii tumezokuelezea, ewe Mtume, ni ukweli wa yakini usio na shaka

96Basi litakase jina la Mola wako Aliyetukuka na umtakase na yale ambayo madhalimu na wenye kukanusha wanayasema. Mwenyezi Mungu Yuko juu ya yale wanayoyasema ujuu mkubwa sana

chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr

WEBREATH · 11:11

«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath