Uislamu
nyuma

53. An-Najm

1Anaapa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa nyota zinapozama zikawa hazionekani

2kwamba Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hakupotoka kwenye njia ya uongofu na haki, na hakutoka nje ya njia ya usawa. Bali yeye yuko kwenye upeo wa unyofu, usawa na uthabiti

3Kutamka kwake hakutokani na matamanio ya nafsi yake. Haikuwa

4Qur’ani na haikuwa Sunnah isipokuwa ni wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Nabii Wake Muahammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

5Alimfundisha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Malaika mwenye nguvu nyingi

6mwenye mandhari mazuri, naye ni Jibrili, amani imshukie, aliyejitokeza kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

7na akalingana kwa umbo lake la kihakika, kwenye pembe za sehemu za juu, nao ni pembe za jua linapochomoza

8Kisha Jibrili akakaribia kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie

9na akazidi kukaribia mpaka ikawa kukaribia kwake ni kiasi cha nyuta mbili au karibu zaidi

10Hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, alimpelekea wahyi mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kile alichokituma kwa wahyi kupitia Jibrili, amani imshukie

11Haukukanusha moyo wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kile alichokiona kwa macho yake

12Je mnamkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amni zimshukie, mkajadiliana naye juu ya kile alichokiona na kukishuhudia miongoni mwa alama za Mola wake

13Na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alimuona Jibrili, kwa sura zake za uhakika Alizomuumba nazo Mwenyezi Mungu

14mara nyingine hapo penye Sidrah al-Muntahā- mti wa mkunazi ulio kwenye uwingu wa saba ambapo hapo kinakomea kinachopanda juu kutoka ardhini na kinakomea kinachoshuka chini kutoka juu yake

15Mbele ya mti huo kuna Pepo ya al- Ma’wā (Makazi ya Daima) ambayo waliahidiwa wachamungu

16Pindi huo Mkunazi ulipofinikwa kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu na kitu kikubwa hakuna ajuaye sifa zake isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka

17Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikuwa na sifa kubwa ya uthabiti na utiifu, hayakupotoka macho yake kuliani wala kushotoni, wala hakupitisha zaidi ya kile alichoamrishwa kukiona

18Hakika Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, aliona, usiku wa Mi'rāj (kwenda mbinguni) alama kubwa zinazojulisha uweza wa Mwenyezi Mungu na ukubwa Wake miongoni mwa Pepo, Moto na vinginevyo

19Mnawaonaje, enyi washirikina, waungu hawa mnaowaabudu: Lāta, 'Uzzā

20na mwingine wa tatu ni Manātu, je hao wamenufaisha au kudhuru mpaka wawe ni washirika wa Mwenyezi Mungu

21Je huyu mwanamume mnamfanya ni wenu kwa kuwa mnaridhika naye, na mwanamke ambaye hamridhiki naye nyinyi wenyewe mnamfanya ni wa Mwenyezi Mungu

22Hiko ni kigawanyo cha kidhalimu. Hawakuwa hawa masanamu isipokuwa majina yasiyokuwa na sifa zozote za ukamilifu

23Hayo si chochote isipokuwa ni majina mliyoyaita nyinyi na baba zenu kulingana na matamanio yenu yaliyo batili, Mwenyezi Mungu hakuteremsha ushahidi wowote wa kusadikisha madai yenu juu ya hayo. Hawafuati hawa washirikina isipokuwa dhana na matamanio ya nafsi zao zilizopotoka zikawa kando na maumbile ya sawa. Na hakika yaliwajia wao kutoka kwa Mola wao, kwa ulimi wa Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yale ambayo ndani yake pana uongofu wao, na wao hawakunufaika nao

24Binadamu hatapata kile anachokitamani cha kuwa waabudiwa hawa au wasiokuwa hawa, katika vitu vinavyotamaniwa na nafsi yake, watamuombea

25Basi ni ya Mwenyezi Mungu amri ya duniani na Akhera

26Na kuna Malaika wengi huko mbinguni, pamoja na vyeo vyao vya juu, kuombea kwao hakunufaishi chochote isipokuwa baada ya Mwenyezi Mungu kuwapa idhini wao waombee na Aridhike na yule mwenye kuombewa

27Hakika wale ambao hawaamini kuwa kuna maisha ya Akhera miongoni mwa makafiri wa Kiarabu wala hawafanyi matendo ya kuwafaa huko, wanawaita Malaika vile wanavyowaita wanawake, kwa kuitakidi kwao kuwa Malaika ni wanawake na kuwa wao ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu

28Na wao hawana ujuzi wowote ulio sahihi, kuhusu jambo hilo, wenye kusadikisha hayo waliyoyasema. Hawafuati isipokuwa dhana ambayo haifalii kitu na haisimami kabisa mahali pa haki

29Basi mpuuze yule anaoupa mgongo utajo wetu, nao ni Qur’ani, na asitake chochote isipokuwa uhai wa kilimwengu

30Hali hiyo waliyonayo ndio upeo wa ujuzi wao na lengo lao. Hakika Mola wako Ndiye Anayemjua zaidi aliyepotoka kutoka kwenye njia ya uongofu, na Yeye ndiye Anayemjua zaidi aliyeongoka na akafuata njia ya Uislamu.. Hapa pana onyo kali kwa wenye kuasi na kukataa kukitumia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kufuata mwenendo wa Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wenye kufadhilisha matamanio ya nafsi na hadhi za ulimwenguni juu ya Akhera

31Ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, mamlaka ya vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, ili Awalipe wale waliokosa kwa kuwatesa kwa maovu waliyoyafanya na Awalipe Pepo wale waliofanya wema

32nao ni wale wanaojiepusha na madhambi makubwa na machafu isipokuwa dhambi ndogondogo nazo ni dhambi ndogo ambazo haendelei nazo mwenye kuzifanya, au zile ambazo mja amezifanya kwa nadra. Kwani hizo pamoja na kufanya mambo ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, Atayasamehe nayo Mwenyezi Mungu na Atawasitiria. Hakika Mola wako ni Mkunjufu wa msamaha. Yeye Anazijua zaidi hali zenu Alipomuumba baba yenu Ādam kwa mchanga, na mlipokuwa bado hamjazaliwa, mko ndani ya matumbo ya mama zenu. Basi msizitakase nafsi zenu, mkazipamba na mkazipa sifa za uchamungu. Yeye Anamjua zaidi anayeogopa mateso Yake miongoni mwa waja Wake na akajiepusha na kufanya mambo ya kumuasi

33Unamuonaje, ewe Mtume, yule anayekataa kumtii Mwenyezi Mungu

34na akatoa kidogo katika mali yake kisha akaacha kutoa na akakata hisani yake

35Je huyu anayekata kheri yake ya kutoa ana ujuzi wa ghaibu kuwa yeye atamalizikiwa na mali yaliyoko mkononi mwake ndipo akaizuia kheri yake asiitoe, na akawa aliona hilo waziwazi? Mambo si hivyo! Hakika ni kwamba yeye aliacha kutoa sadaka na kufanya kheri, kutenda wema na kuunga kizazi kwa ubahili na uchoyo

36Kwani hakupewa habari ya yaliyomo ndani ya kurasa za Taurati

37na nyaraka za Ibrāhīm aliyetekeleza kile alichoamrishwa na akakifikisha

38Kwamba haipatilizwi nafsi yoyote kwa kosa la nafsi nyingine, na mzigo wake hakuna yoyote atakayembebea

39Na kwamba binadamu hapewi malipo isipokuwa kwa kile alichokichuma yeye mwenyewe kwa juhudi zake

40Na kwamba juhudi zake zitaonekana Akhera, yapambanuliwe mazuri yake na mabaya yake, ili kumkirimu mtenda wema na kumlaumu mfanya mabaya

41kisha binadamu atalipwa kwa juhudi zake malipo yenye kuenea kikamilifu matendo yake yote

42Na kwamba kwa Mola wako, ewe Mtume, ndipo watakapokomea viumbe Vyake vyote Siku ya Kiyama

43Na kwamba Yeye, Aliyetukuka na kutakasika, Ndiye Anayemfanya Anayemtaka acheke duniani kwa kumfurahisha, na ndiye Anayemfanya Anayemtaka alie kwa kumpa makero

44Na kwamba Yeye Ndiye Anayemfisha Anayetaka afe miongoni mwa vuimbe Vyake na Ndiye Anayemuhuisha Anayetaka ahuike miongoni mwao. Basi Yeye Ndiye Aliyepwekeka, kutakasika ni Kwake, kwa kuhuisha na kufisha

45Na kwamba Yeye Ameumba jinsi mbili: ya kiume na ya kike, kati ya wanadamu na wanyama

46kutokana na tone la manii linalomiminwa kwenye kizazi

47Na kwamba ni juu ya Mola wako, ewe Mtume, kurejesha uumbaji wao baada ya kufa kwao, na huo ndio uumbaji mwingine Siku ya Kiyama

48Na Yeye Ndiye Anayewatajirisha Anaowataka miongoni mwa viumbe Wake kwa mali, na Ndiye Anayewamilikisha na kuwaridhisha nayo

49Na kwamba Yeye Ndiye Mola wa al-Shi'rā, nayo ni nyota inayong’ara ambayo baadhi ya watu wa zama za Ujinga walikuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu

50Na kwamba Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, Aliwaangamiza 'Ād wa mwanzo, nao ni watu wa Hūd

51Na Akawaangamiza Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, Asimbakishe yoyote katika wao

52Na Akawaangamiza watu wa Nūḥ hapo kabla. Hao walikuwa ni wakali zaidi wa uasi na wakubwa zaidi wa ukafiri kuliko wale waliokuja baada yao

53Na miji ya watu wa Lūṭ, Mwenyezi Mungu Aliipindua juu yao Akazifanya sehemu za juu yake kuwa chini yake

54na Akaifinika mawe yaliyowateremkia kwa mfululiza kutoka juu kama mvua

55Basi ni neema zipi za Mola wako, ewe binadamu mkanushaji, unazifanyia shaka

56Huyu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mwonyaji wa haki ambayo kwayo walionya Manabii kabla yake, si kitu kipya katika Mitume

57Kiyama kimekaribia na wakati wake umekaribia

58Hivyo basi hakuna yoyote mwenye kukizuia isipokuwa Mwenyezi Mungu, na hakuna mwenye kujua wakati wa kufika kwake isipokuwa Mwenyezi Mungu

59Je hii Qur’ani mnaionea ajabu, enyi washirikina, kuwa ni sahihi

60Na mnaicheka kwa shere nastihzai na hamlii kwa kuogopa maonyo yake

61na hali nyinyi mnapumbaa na mmeipa mgongo

62Basi msujudieni Mwenyezi Mungu na mtakasieni Ibada Yeye Peke Yake, Na mumuachie Yeye mambo yenu

chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr

WEBREATH · 11:11

«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath