Uislamu
nyuma

52. At-Tur

1Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Ṭūr, nalo ni jabali ambalo juu yake Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Alizungumza na Mūsā

2Na kwa Kitabu kilichoandikwa, nacho ni Qur’ani

3kwenye nyaraka zilizokunjuliwa

4Na kwa Nyumba Iliyoamirishwa kwa Malaika watukufu wenye kuizunguka daima

5Na kwa sakafu iliyoinuliwa juu, nayo ni uwingu wa duniani

6Na kwa bahari iliyowashwa moto, iliyojaa maji

7Hakika adhabu ya Mola Wako, ewe Mtume, ni yenye kuwashukia makafiri

8Hakuna kizuizi cha kuizuia itakaposhuka

9Siku ya mbingu kutetemeka mpango wake kuharibika na pande zake kusukikasukika, na hapo ni wakati wa mwisho wa dunia

10na majabali yaondoke mahali pake na yatembee kama vile mawingu yanavyotembea

11Maangamivu katika Siku hii ni yenye kuwashukia wakanushaji

12Ambao wao wamevama ndani ya ubatilifu wanapumbaa nao na wanaifanya dini yao kuwa ni shere na mchezo

13Siku ya kusukumwa hawa wakanushaji msukumo wa nguvu wenye kuwadhalilisha hadi kwenye Moto wa Jahanamu

14Na waambiwe kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia, «Huu ndio huo Moto ambao mlikuwa mkiukanusha

15«Je, ni uchawi adhabu hii mnayoishuhudia au nyinyi hamtazami

16Onjeni ukali wa Moto huu. Vumilieni uchungu wake na ukali wake au msiyavumilie hayo, hamtahafifishiwa adhabu na hamtatoka humo. Ni sawasawa kwenu nyinyi mkivumilia au mkitovumilia. Hakika nyinyi mnalipwa tu yale mliokuwa mkiyafanya duniani

17Hakika wachamungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo na neema kubwa

18Watajistarehesha kwa vile Alivyowapa Mwenyezi Mungu vya neema miongoni mwa aina mbalimbali za ladha na starehe, na Atawaokoa mwenyezi Mungu kutokana na adhabu ya Moto

19Kuleni chakula kwa furaha, na mnywe kinywaji chenye ladha, yakiwa ni malipo ya matendo mema mliyoyafanya duniani

20Na wao watakuwa wametegemea, wako juu ya vitanda vinavyoelekeana, na tutawaoza wanawake weupe wenye macho mapana yaliyo mazuri

21Na wale walioamini na wakafuatwa na watoto wao katika hiyo Imani, Tutawakutanisha watoto wao nao katika daraja yao Peponi, hata kama hawakufikia matendo ya wazazi wao, ili wazazi wafurahike na watoto wao pamoja na wao katika daraja zao. Watakusanywa baina yao kwenye hali nzuri zaidi, na hatutawapunguzia chochote katika matendo yao mema. Kila mtu anafungwa na matendo yake aliyoyachuma, hatobeba dhambi za watu wengine

22Na tutawaongezea, juu ya starehe hizo zilizotajwa, matunda na nyama miongoni mwa vitu vinavyopendwa na kutamaniwa

23Na miongoni mwa starehe hizo ni kuwa wao watapeana gilasi ya pombe, mmoja wao atampa mwenzake, ili furaha yao ikamilike. Kinywaji hiki kinatafautiana na pombe ya duniani, hakimleweshi akili mwenye kukinywa, wala hakisababishi kubobokwa, wala maneno ya makosa na maasia

24Na watawazunguka watumishi waliotayarishwa kuwatumikia kama kwamba wao katika usafi na weupe na utungaji nidhamu ni lulu iliyohifadhiwa kwenye mashaza yake

25Watageukiana watu wa Peponi kuulizana wao kwa wao juu ya ukubwa wa yale waliyonayo na sababu ya kuyapata

26Watasema, «Sisi tulikuwa kabla, huko duniani, na sisi tuko baina ya watu wetu, tunamuogopa Mola wetu, tuna hadhari na adhabu Yake na mateso yake Siku ya Kiyama

27Mwenyezi Mungu Akatuneemesha kwa uongofu na taufiki na Akatuokoa na adhabu ya vuke la Jahanamu, nalo ni moto wake na joto lake. Sisi tulikuwa, hapo kabla, tukimnyenyekea Yeye Peke Yake, hatumshirikishi na Yeye yoyote asiyekuwa Yeye, Atulinde na adhabu ya vuke la Motoni na Atupeleke kwenye starehe ya Peponi

28Mwenyezi Mungu Akatukubalia maombi yetu, na Akatupa tulichokiomba. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa kheri, Mwenye kurehemu. Na miongoni mwa wingi wa kheri Zake na rehema Zake kwetu ni kule kutupa radhi zake na Pepo, na kutuepusha na hasira Zake na Moto.»

29Basi wawaidhie, ewe Mtume, wale uliotumilizwa kwao kwa Qur’ani, kwani hukuwa wewe, kwa neema ya Mwenyezi Mungu Aliokuneemesha kwayo ya unabii na busara ya akili, ni kuhani anayetoa habari za ghaibu bila ujuzi wala mwendawazimu asiyejua analolisema, kama wanavyodai

30Au wanakwambia hao washirikina, ewe Mtume, «Yeye ni mshairi, tunangojea ashukiwe na mauti»

31Waambie, «Yangojeeni mauti yangu, kwani mimi pamoja na nyinyi ni katika wenye kuingojea adhabu yenu, na mtaona ni nani atakayekuwa na mwisho mwema

32Au zinawaamuru akili zao, hao wakanushaji, ziseme neno hili linalogongana (kuwa sifa ya ukuhani, utungaji mashairi, na wendawazimu haiwezekani kukutana wakati mmoja)? Bali wao ni watu waliruka mipaka katika uasi

33Au wanasema hawa washirikina, «Muhammad Ameibuni Qur’ani yeye mwenyewe?» bali wao hawaamini. Na lau wangaliamini, hawangalilisema walilolisema

34Basi na walete maneno mfano wa Qur’ani iwapo wao ni wakweli katika madai yao kuwa Muhammad Ameibuni

35Je, wameumbwa hawa washirikina bila kuwako mwenye kuwaumba na kuwapatisha au wao wamejiumba wenyewe? Na yote mambo mawili haya yametanguka na hayawezekani. Na kwa hivyo, inalazimika kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba, na Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye hakuna anayepasa kuabudiwa, wala kufaa kuabudiwa, isispokuwa Yeye

36Au wao wameumba mbingu na ardhi kwa utengezaji huu wa kipekee? Bali wao hawaamini adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao ni washirikina

37Au wanazo wao hazina za Mola wako wanazitumia? Au wao ni majebari wanaowagandamiza viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa kuwatendesha nguvu na kuwanyanyasa? Mambo si hivyo, bali wao ndio walemevu walio madhaifu

38Au wao wana ngazi ya kupandia mbinguni wanasikiliza huko wahyi kwamba yale waliyonayo ndio haki? Basi na aje, yule anayedai kuwa amesikia hilo, na hoja ya waziwazi yenye kusadikisha madai yake

39Je, mwenyezi Mungu , aliyetakasika, Ana watoto wa kike na nyinyi mna watoto wa kiume kama mnavyodai kwa uzushi na urongo

40Au je unawataka, ewe Mtume, hawa washirikina wakupatie malipo ya kuwafikishia Ujumbe, wakawa wao wana tabu na dhiki ya kujilazimisha malipo unayoyataka kutoka kwao

41Au je wao wana ujuzi wa ghaibu wakawa wanawaandikia watu na kuwapa habari yake? Mambo si hivyo, kwani hakika ya mambo ni kwamba hakuna anayejua ghaibu iliyo mbinguni na ardhini isipokuwa Mwenyezi Mungu

42Bali wao wanataka kumfanyia vitimbi Mtume wa Mwenyezi Mungu na Waumini. Basi hao makafiri, vitimbi vyao na njama zao vitawarudia wao wenyewe

43Au wao wana muabudiwa anayestahiki kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu? Ametakasika Mwenyezi Mungu na kutukuka na yale wanayoshirikisha. Kwani Yeye Hana mshirika katika mamlaka, na Hana mshirika katika Upweke na ustahiki wa kuabudiwa

44Na wakikiona hawa washirikina kipande cha mbingu kinawaangukia, kikiwa ni adhabu kwao, hawataacha yale waliyo nayo ya ukanushaji, na watasema, «Haya ni mawingu yamekusanyika na kupandana.»

45Basi waache, ewe Mtume, hawa washirikina mpaka wakutane na Siku yao hiyo ya wao kuangamizwa, nayo ni Siku ya Kiyama

46Katika Siku hiyo havitawazuilia wao vitimbi vyao kotokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu kitu chochote, na hatawanusuru yoyote kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

47Hakika madhalimu hawa watakuta adhabu duniani, kabla ya adhabu ya Siku ya Kiyama, ya kuuawa, kukamatwa mateka, adhabu ya kaburini na nyinginezo. Lakini wengi wa watu hawajui hilo

48Na uivumilie, ewe Mtume, hukumu ya Mola wako na amri Yake juu ujumbe Aliyokubebesha na juu ya makero yanayokupata kutoka kwa watu wako, hakika wewe uko kwenye maangalizi yetu, hifadhi na utunzi. Na umtakase Mola Wako kwa kumsifu unaposimama kuswali na unapoinuka kutoka usingizini

49Na kwenye kipindi cha usiku mtakase Mola wako kwa kumsifu, umtukuze na umswalie. Na ufanye hayo kwenye kipindi cha Swala ya Asubuhi wakati wa nyota kuondoka. Katika aya hizi pana kuthibitisha sifa ya macho mawili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa inavyonasibiana na Yeye, bila kufananisha na viumbe Vyake au kuieleza dhati Yake vile ilivyo, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake na sifa njema zote ni Zake, kama lilivyothibiti hilo katika Sunnah na kukubaliana juu yake wanavyuoni waliopita wa Ummah huu

chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr

WEBREATH · 11:11

«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath