26. Ash-Shu'araa
1«Ṭā, Sīn, Mīm.» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato mwanzo wa sura ya Al-Baqarah
2Hizi ni aya za Qur’ani yenye kufafanua kila kitu, yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu
3Huenda wewe, ewe Mtume, kwa kuwa una hamu sana ya kutaka wao waongoke, ukajiangamiza mwenyewe kwa kuwa wao hawakukuamini na hawakufuata kimatendo uongofu wako. Basi usifanye hivyo
4Tukitaka tutawateremshia wakanushaji, miongoni mwa watu wako, miujiza itokayo mbinguni yenye kuwaogopesha itakayowalazimisha wao kuamini, na hapo shingo zao ziwe zimenyongeka na kudhalilika. Lakini hatukutaka hilo, kwani Imani yenye kunufaisha ni kuyaamini yaliyoghibu kwa hiyari
5Na hauwajii washirikina hawa ukumbusho, kutoka kwa Mwingi wa rehema unaoanzwa kuteremshwa, kitu baada ya kitu, wenye kuwaamrisha na kuwakataza na kuwakumbusha Dini ya kweli, isipokuwa wanaupa mgongo na hawaukubali
6Kwa hakika washaikanusha Qur’ani na washaifanyia shere, basi zitawajia wao habari za jambo ambalo walikuwa wakilifanyia shere na dharau, na itawashukia wao adhabu ikiwa ni malipo ya kumuasi Mola wao
7Je, wanakanusha na hali wao hawakuiangalia ardhi ambayo ndani yake tumeotesha kila aina nzuri ya mimea ambayo hakuna awezae kuiyotesha isipokuwa Mola wa viumbe vyote
8Kwa hakika, katika kuitoa mimea kwenye ardhi ni dalili wazi ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, na wengi wa watu hawakuwa ni wenye kuamini
9Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi wa kila kiumbe, ni Mwenye kurehemu Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu
10Na wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi Mola wako Alipomuita Mūsā kuwa awaendee watu madhalimu
11nao ni watu wa Fir’awn na uwaambie wayaogope mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na waache ukafiri na upotevu walionao
12Mūsā akasema, «Mola wangu! Mimi ninaogopa wasije wakanikanusha juu ya utume
13na moyo wangu ukaingia kero kwa kunikanusha, na ulimi wangu usiwe na ufasaha wa kulingania. Basi mtume Jibrili aende na wahyi kwa ndugu yangu Hārūn, ili anisaidie na aniamini kwa ninayoyasema, na awafafanulie kile ninachowaambia, kwani yeye ana ufasaha zaidi wa matamshi kuliko mimi
14Na watanishika na kosa la kumuua mwanamume wa jamii ya Qibṭī miongoni mwao, na kwa hivyo ninaogopa wasiniue kwa ajili yake.»
15Mwenyezi Mungu Akamwambia Mūsā, «Sivyo hivyo! Hawatakuua. Na nimekubali matakwa yako juu ya Hārūn. Basi endeni mkiwa na miujiza yenye kuonyesha ukweli wenu. Sisi tuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi, utunzi na usaidizi tunasikiliza
16Mjieni Fir’awn na mumwambie, «Sisi tumetumwa kwako na kwa watu wako kutoka kwa Mola wa viumbe wote
17kwamba uwaache Wana wa Isrāīl waende na sisi.»
18Fir’awn akasema kumwambia Mūsā kwa kumsimanga, «Je, hatukukulea kwenye majumba yetu ukiwa mchanga, ukakaa kwenye utunzi wetu miaka (mingi) katika umri wako
19ukafanya tendo la jinai kwa kumuua mwanamume miongoni mwa watu wangu, ulipompiga na ukamsukuma, na wewe ni miongoni mwa wakanushaji neema zangu na kukataa uola wangu
20Mūsā akasema kumjibu Fir’awn, «Nilifanya uliyoyataja kabla Mwenyezi Mungu Hajaniletea wahyi na kunitumiliza kama Mtume
21ndipo nilitoka kwenu kwa kukimbia kuelekea Madyan nilipoogopa usije ukaniua kwa nililolifanya bila kukusudia, Na Mola wangu Akanitunuku unabii na elimu na Akanifanya ni miongoni mwa Mitume
22Na kwani huko kulelewa nyumbani kwako unakuona ni neema kutoka kwako juu yangu, na hali wewe umewafanya Wana wa Isrāīl ni watumwa , unawachinja wana wao wa kiume na unawaachilia wanawake wao ili watumwe na wadharauliwe?»
23Fir’awn akamwambia Mūsā, «Na huyo Mola wa viumbe wote Ambaye unadai kwamba wewe ni mjumbe Wake, ni kitu gani?»
24Mūsā akasema, «Yeye ni Mmiliki na Mwenye kuipelekesha mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya viwili hivyo. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi aminini.»
25Fir’awn akasema kuwaambia walioko pambizoni mwake miongoni mwa watukufu wa watu wake, «Je, hamusikii maneno ya Mūsā ya ajabu kwamba kuna mola asiyekuwa mimi?»
26Mūsā akasema, «Mola Ambaye mimi nawalingania nyinyi Kwake ni Yule Aliyewaumba nyinyi na Aliyewaumba wa mwanzo. Basi vipi nyinyi mnamuabudu ambaye ni kiumbe kama nyinyi na yeye ana mababa waliotoeka kama mababa zenu?»
27Fir’awn akasema kuwaambia wale watu wake makhsusi akiwapandisha ghadhabu zao, kwa kuwa Mūsā amemkanusha yeye, «Kwa kweli, huyu mjumbe wenu aliyeletwa kwenu ni mwendawazimu , asema maneno yasiyofahamika.»
28Mūsā akasema, «Mola wa Mashariki na Magharibi na vilivyoko baina ya viwili hivyo, na vilivyomo ndani yake vya mwangaza na giza. Hili linapelekea kuwa ni lazima kumuamini Yeye Peke Yake, iwapo nyinyi ni miongoni mwa watu wa akili na kuzingatia.»
29Fir’awn akamwambia Mūsā kwa kumtisha, «Ukichukua mwingine aseyekuwa mimi ukamfanya ni mola nitakufunga jela pamoja na wale niliowafunga.»
30Mūsā akasema, «Je, utanifanya mimi ni miongoni mwa wafungwa jela, hata nikikuletea hoja ya kukata ambayo kwa hiyo utabainika ukweli wangu?»
31Fir’awn akasema, «Basi ilete ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika madai yako.»
32Hapo Mūsā akaitupa fimbo yake na ikageuka kuwa nyoka wa kikweli, si kiinimacho kama wanavyofanya wachawi
33Na akautoa mkono wake kwenye uwazi wa kanzu yake uliofunguliwa kifuani au chini ya kwapa lake, na papo hapo ukawa mweupe kama barafu, na sio weupe wa mbalanga, ukawashangaza waangaliaji
34Fir’awn akasema kuwaambia watukufu wa watu wake, kwa kuogopa wasije wakaamini, «Kwa kweli Mūsā ni mchawi hodari
35Anataka kuwatoa nyinyi, kwa uchawi wake, kwenye ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani kuhusu yeye nipate kuyafuata maoni yenu?»
36Watu wake wakamwambia, «Msubirishe Mūsā na Hārūn, na utume askari mijini wawakusanye wachawi
37Watakujia na kila anayejua uchawi na akawa hodari kuufahamu.»
38Wakakusanywa wachawi, na wakapangiwa wakati maalumu, nao ni wakati wa mchana wa siku ya Pambo ambayo wanajitenga na shughuli zao, na wanajikusanya na kujipamba, ili wakutane na Mūsā
39na wawahimize watu kujumuika kwa matarajio kwamba ushindi uwe ni wa wachawi
40Sisi tunatarajia ushindi uwe ni wa wachawi ili tujikite kwenye dini yetu
41Na wachawi walipomjia Fir’awn walimwambia, ‘Je, sisi tutakuwa na malipo ya mali au heshima ikiwa tutakuwa ni wenye kumshinda Mūsā?»
42Fir’awn akasema, «Ndio, nyinyi mtapata kwangu malipo mnayoyataka, na nyinyi hapo mtakuwa ni miongoni mwa wenye kusogezwa karibu na mimi.»
43Mūsā akasema kuwaambia wachawi, akitaka kuutangua uchawi wao na kuonyesha kuwa kile alichokileta si uchawi, «Tupeni mtakavyovitupa vya uchawi.»
44Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na zikawadhihirikia watu kwenye akili zao kuwa ni nyoka wanaotembea, na wakaapa kwa enzi ya Fir’awn kwa kusema, «Sisi ni wenye kushinda.»
45Hapo akaitupa Mūsā fimbo yake, na papo hapo ikawa ni nyoka mkubwa, akawa anavimeza vile vilivyotokana na wao, hao wachawi, vya uzushi na bandia
46Waliposhuhudia hilo na wakajua kuwa halitokani na udanganyifu wa wachawi, walimuamini Mwenyezi Mungu na wakamsujudia
47na wakasema, «Tumemuamini Mola wa viumbe vyote
48Mola wa Mūsā na Hārūn.»
49Fir’awn akasema kuwaambia wachawi kwa kukataa, «Mumemkubali Mūsā bila ya idhini yangu!» Na akasema akiashiria kuwa kitendo cha Mūsā ni uchawi, «Yeye ni mkubwa wenu aliyewafundisha nyinyi uchawi, basi mtayajua mateso yatakayowafikia. Nitaikata mikono yenu na miguu yenu kitafauti: kwa kuukata mkono wa kulia na mguu wa kushoto au kinyume chake, na nitawasulubu nyote.»
50Wachawi walisema kumwambia Fir’awn, «Hakuna madhara ya duniani yatakayotupata, kwa kweli sisi ni wenye kurudi kwa Mola wetu, Atupe neema ya kuendelea
51Sisi tunataraji Mola wetu Atusamehe makosa yetu ya ushirikina na mengineyo kwa kuwa sisi ndio Waumini wa mwanzo katika watu wako.»
52Na Mwenyezi Mungu Akampelekea wahyi Mūsā, amani imshukie, kwamba, «Enda usiku pamoja na walioamini miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ili Fir’awn na askari wake, ambao watawafuata nyinyi, wasije wakawafikia kabla ya kufika kwenu baharini.»
53Fir’awn akawatuma askari wake, alipopata habari kwamba Wana wa Isrāīl wameenda usiku, wakusanye jeshi lake kutoka miji ya utawala wake
54Fir’awn akasema, «Kwa kweli, Wana wa Isrāīl waliokimbia pamoja na Mūsā ni pote twevu lenye idadi ndogo
55Na wao wamevijaza hasira vifua vyetu kwa kuwa wameenda kinyume na dini yetu na wametoka bila ya idhini yetu
56na sisi sote tuko macho, tuko tayari nao.»
57Mwenyezi Mungu Akamtoa Fir’awn na watu wake kwenye ardhi ya Misri yenye mabustani, mabubujiko ya maji
58hazina za mali na majumba mazuri
59Na kama tulivyowatoa, tuliwapatia nyumba hizo Wana wa Isrāīl baada yao wao
60Hivyo basi Fir’awn na askari wake walimkuta Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wakati wa kuchomoza jua
61Yalipoonana makundi mawili, watu wa Mūsā walisema, «Kwa hakika jumuiko la Fir’awn ni lenye kutufikia na kutuangamiza.»
62Mūsā alisema kuwaambia, «Sivyo! Mambo si kama mlivyotaja. Hamtafikiwa. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Yupo na mimi kwa msaada, Ataniongoza njia ya kuokoka mimi na kuokoka nyinyi.»
63Hapo tukampelekea wahyi Mūsā kwamba, «Piga bahari kwa fimbo yako!» Akapiga. Na bahari ikapasuka njia kumi na mbili kwa idadi ya kabila za Wana wa Isrāīl. Na kila kipande kilichojitenga na bahari ni kama jabali kubwa
64Na tulimsogeza karibu Fir’awn na watu wake mpaka wakaingia baharini
65Na tukamuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote. Bahari ikaendelea kuachana kwake (kwa ule mpasuko) mpaka wakavuka kwenye nchi kavu
66Kisha tukamzamisha Fir’awn na waliokuwa pamoja na yeye kwa kuifanya bahari iwafinike baada ya wao kuingia ndani wakimfuata Mūsā na watu wake
67Kwa hakika, katika hilo lililotukia pana mazingatio ya ajabu yenye kuonyesha dalili ya uweza wa Mwenyezi Mungu. Na wengi wa wafuasi wa Fir’awn hawakuwa ni wenye kuamini, pamoja na alama hii yenye kushinda
68Na hakika ya Mola wako Ndiye Mshindi, Ndiye Mwenye kurehemu. Kwa nguvu Zake na ushindi Amewaangamiza makafiri wakanushaji, na kwa rehema Yake Amemuokoa Mūsā na waliokuwa pamoja na yeye wote
69Na wasimulie makafiri, ewe Mtume, habari ya Ibrāhīm
70alipomwambia babake na watu wake, «Mnaabudu kitu gani?»
71Wakasema, «Tunaabudu masanamu, tunaketi na kuendelea kuwaabudu.»
72Akasema Ibrāhīm akiwatanabahisha uharibifu wa njia yao, «Kwani wanasikia maombi yenu mnapowaomba
73Au wanawapatia manufaa mkiwaabudu? Au wanawafanya mupate madhara mkiacha kuwaabudu?»
74Wakasema, «Haliwi lolote katika hayo, lakini tuliwakuta mababa zetu wakiwaabudu, na sisi tukawaiga katika yale ambayo walikuwa wakiyafanya.»
75Ibrāhīm akasema, «Je, mumefikiria kuvitia akilini hivyo mnavyoviabudu, miongoni mwa masanamu yasiyosikia wala kunufaisha wala kudhuru
76nyinyi na mababa zenu waliowatangulia
77Kwani hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni maadui zangu. Lakini Mola wa viumbe wote na Mmiliki wa mambo yao, Yeye Peke Yake Ndiye ninayemuabudu
78Yeye Ndiye Aliyeniumba kwa sura nzuri zaidi. Yeye ananiongoza kwenye maslahi ya dunia na Akhera
79Na Yeye Ndiye Anayenineemesha kwa chakula na kinywaji
80Na nikipatikana na ugonjwa, Yeye Ndiye Anayeniponyesha na kuniondolea
81Na Yeye Ndiye Atakayenifisha duniani kwa kuichukua roho yangu, kisha Atanihuisha Siku ya Kiyama, hakuna awezaye hilo isipokuwa Yeye
82Na Ambaye ninatarajia Atanisamehe dhambi zangu Siku ya Malipo.»
83Ibrāhīm akasema akimuomba Mola wake, «Mola wangu! Nitunukie elimu na fahamu, na unikutanishe na watu wema, na unikusanye mimi na wao Peponi
84«Na unifanye niwe na sifa nzuri na utajo mwema kwa wale watakaokuja baada yangu mpaka Siku ya Kiyama
85«Na unifanye mimi niwe miongoni mwa waja wako utakaowarithisha starehe za Peponi.»
86Hii ni dua ya Ibrāhīm, amani imshukiye, ya kumuomba Mwenyezi Mungu Amuokoe babake na upotevu na Ampe uongofu, ili Amghufirie na Amsamehe, kama Ibrāhīm alivyomuahidi babake kumuombea Mungu, na ilipomfunukia kuwa yeye ni mwenye kuendelea kwenye ukafiri na ushirikina mpaka afe alijiepusha naye
87«Na usinipe unyonge Siku hiyo, ambayo watu watatoka makaburini ili wahesabiwe na walipwe
88Siku ambayo mali na watoto havitamfaa yoyote miongoni mwa waja
89isipokuwa yule aliyemjia Mwenyezi Mungu kwa moyo uliyosalimika na ukafiri, unafiki na uovu.»
90Na Pepo itasogezwa karibu kwa wale waliojiepusha na ukafiri na matendo ya uasi na wakamuelekea Mwenyezi Mungu kwa kumtii
91Na Moto utaonyeshwa waziwazi kwa makafiri ambao walipotea njia ya uongofu na wakayafanyia ujasiri yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake
92Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu
93badala ya Mwenyezi Mungu na mkidai kwamba wao watawaombea leo? Je, watawanusuru na wawazuilie adhabu isiwafikie au watajinusuru kwa kuikinga adhabu isiwafikie?» Hakuna chochote katika hayo
94Hapo watakusanywa na watupwe kwenye Jahanamu kwa vichwa vyao, mara baada ya nyingine mpaka watakapotulia humo: wao, wale waliowapoteza
95na wasaidizi wa Iblisi waliowapambia shari; hakuna yoyote kati yao atakayeponyoka
96Watasema wakikiri makosa yao, na huku wanagombana, ndani ya Jahanamu, na wale waliowapoteza wao
97«Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba sisi, duniani, tulikuwa kwenye upotevu ulio waziwazi, haukuwa umefichika
98tulipowafanya nyinyi kuwa ni sawa na Mola wa viumbe wote, Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake
99Na hakuna kilichotutia kwenye mwisho huu mbaya isipokuwa ni wahalifu ambao walitulingania tumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu
100«Hapana yoyote wa kutuombea na kututoa kwenye adhabu
101wala mwenye kutupenda kikweli na kutuhurumia
102«Tunatamani tupatiwe fursa ya kurudi ulimwenguni tupate kuwa miongoni mwa wenye kuamini na kuokolewa.»
103Hakika katika habari ya Ibrāhīm iliyotangulia kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na wengi wenye kuisikia habari hii hawakuwa ni wenye kuamini
104Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Mshindi Aliye Muweza wa kuwalipiza wakanushaji, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini
105Waliukanusha watu wa Nūḥ ujumbe wa Nabii wao. Wakawa, kwa kufanya hivyo, ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa kila Mtume anaamrisha kuwaamini Mitume wote
106Kumbuka pindi aliposema kuwaambia wao ndugu yao Nūḥ, «Je, hamumuogopi Mwenyezi Mungu kwa kuacha kumuabudu asiyekuwa Yeye
107Mimi kwenu nyinyi ni Mtume muaminifu katika yale ninayowafikishia
108Basi ifanyeni Imani kuwa ndio kinga yenu na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumuabudu Yeye Peke Yake
109na sitaki kutoka kwenu malipo yoyote ya kuufikisha ujumbe, malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote, Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake
110Basi jihadharini na mateso Yake na mnitii mimi kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake.»
111Watu wake wakamwambia, «Vipi tutakuamini na tutakufuata na hali hao waliokufuata ni watu wanyonge na wale wa hali ya chini miongoni mwao?»
112Nūḥ, amani imshukie, aliwajibu kwa kusema, «Sikupewa jukumu la kujua matendo yao. Jukumu nililopewa ni kuwalingania wao kwenye Imani. Na linalozingatiwa ni Imani, na sio cheo, ukoo, kazi na ujuzi wa sanaa
113«Hesabu yao, ili walipwe kwa matendo yao na yaliyomo ndani ya nafsi zao, ni juu ya Mola wangu Anayeona na kujua siri zote. Lau mnatambua hilo hamngalisema maneno haya
114«Na mimi si mwenye kuwafukuza wale wanaouamini ulinganizi wangu, namna itakavyokuwa hali yao, kwa kufuata matakwa yenu, ili mniamini
115Mimi sikuwa isipokuwa ni mwonyaji ambaye onyo lake liko wazi.»
116Hapo watu wa Nūḥ waliacha kubishana na wakaamua kutoa vitisho, hivyo basi wakamuambia, «Usiporudi nyuma, ewe Nūḥ, ukaacha huo ulinganizi wako, utakuwa ni miongoni mwa wenye kuuawa kwa kupigwa mawe.»
117Nūḥ aliposikia neno lao hili, alimuomba Mola wake kwa kusema, «Mola wangu! Kwa hakika watu wangu wameamua kuendelea kunikanusha
118basi amua baina yangu na wao uamuzi wa kumwangamiza mwenye kukataa kukupwekesha na akamkanusha Mtume wako. Na uniokoe mimi, na Waumini walio pamoja na mimi, na adhabu utakayowaadhibu makafiri.»
119Basi tukamuokoa na wale walio pamoja na yeye katika jahazi iliyojazwa aina mbalimabali za viumbe alivyovibeba pamoja na yeye
120Kisha tukawazamisha, baada ya kumuokoa Nūḥ na wale waliokuwa pamoja na yeye, wale waliosalia kati ya wale ambao hawakuamini na wakaukataa ushauri aliyowapa
121Hakika katika maelezo ya Nūḥ na yale yaliyokuwa ya kuokolewa Waumini na kuangamizwa wakanushaji ni alama na ni zingatio kubwa kwa waliokuja baada yao. Na wengi wa wale waliokisikia kisa hiki hawakuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na sheria Zake
122Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi katika kuwatesa waliomkanusha na wakaenda kinyume na amri Yake, Mwenye rehema kwa waja Wake walioamini
123Walimkanusha watu wa kabila la ‘Ād Mtume wao Hūd, amani imshukiye, na kwa hivyo wakawa ni wakanushaji wa Mitume wote, kwa kuwa ulinganizi wao ni mmoja katika misingi yake na malengo yake
124Alipowaambia ndugu yao Hūd, «Je, hamumchi MwenyeziMungu mukamtakasia ibada
125Mimi nimetumwa kwenu niwaongoze na niwaonyeshe njia, ni mtunzi wa ujumbe wa Mwenyezi Mungu, ninaufikisha kwenu kama Alivyoniamrisha Mola wangu
126Basi iogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mnitii mimi katika kile ninachowaitia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu
127na sitaki kutoka kwenu, kwa kuwaongoza nyinyi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, aina yoyote ya malipo. Malipo yangu hayako juu ya yoyote isipokuwa Mola wa viumbe wote
128«Je mnajenga kila mahali palipoinuka jengo refu mkawa mnatazama kutoka hapo na mnawacheza shere wapita njia? Huo ni upuuzi na upitaji kiasi, na hauwaletei nyinyi faida yoyote katika dini au katika dunia
129Na mnafanya majumba imara na ngome zilizojengwa madhubuti, kama kwamba nyinyi mtakaa milele duniani na hamtakufa
130Na mnapomshika mtu kwa nguvu na mkamakinika kumuua au kumpiga, basi mnalifanya hilo kwa kutendesha nguvu hali ya kufanya maonevu
131«Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowalingania, kwani hilo lina nafuu zaidi kwenu
132na mcheni Mwenyezi Mungu Aliyewapa aina mbalimbali za neema zisizofichika kwenu
133Amewapa wanyama hawa: ngamia ng’ombe, mbuzi na kondoo, na Amewapa watoto
134na Amewapa mabustani yenye matunda, na Amewatolea maji kwenye chemchemi zinazopita
135Hūd, amani imshukiye, akasema akiwatahadharisha wao, «Mimi ninaogopa , mkiendelea na yale mliyo nayo ya ukanushaji, uonevu na kuzikufuru neema, asije Mwenyezi Mungu Akawateremshia nyinyi adhabu katika Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa kitisho cha adhabu yake
136Wakamwambia, «Ni sawa kwetu kutukumbusha, kututisha na kuacha kufanya hivyo, hatutakuamini
137Na wakasema, «Haikuwa dini hii tuliyonayo isipokuwa ni dini ya watu wa mwanzo na desturi zao
138na sisi si wenye kuadhibiwa kwa tunalolifanya katika yale ambayo unatuonya nayo ya adhabu.»
139Wakaendelea kumkanusha, na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa upepo wa baridi ulio mkali. Kwa hakika, katika kuangamiza huko kuna mazingatio kwa wanaokuja baada yao, na hawakuwa wengi wao, wale waliokisikia kisa chao, ni wenye kukuamini wewe
140Hakika Mola wako Ndiye Mwenye nguvu, Mshindi kwa anayoyataka ya kuwaangamiza wakanushaji, Mwenye huruma kwa Waumini
141Watu wa kabila la Thamūd waliukanusha ujumbe wa Mtume wao Ṣāliḥ na wakaukanusha mwito wake wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, na kwa hivyo wakawa wamewakanusha Mitume wote, kwa kuwa wao wote wanalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu
142Pindi alipowaambia wao ndugu yao Ṣāliḥ»Je, hamuogopi mateso ya Mwenyezi Mungu, mkampwekesha kwa ibada
143Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye kuutunza ujumbe huu kama nilivyoupokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu
144Basi jihadharini na mateso Yake, Aliyetukuka, na fuateni kile nilichowalingania mkifuate
145Na mimi sitaki malipo kwa kuwashauri na kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote
146«Je, Awaache Mola wenu katika starehe mlizonazo, hali ya kuwa mumetulia katika dunia hii mkiwa mumesalimika na adhabu na kuondoka na kufa
147Mkiwa kwenye mabustani yenye matunda, chemchemi zinazopita
148nafaka nyingi na mitende ambayo matunda yake yamestawi, yamelainika na yameiva
149na mnachonga kutoka kwa majabali majumba hali ya kuwa ni wamahiri wa kuyachonga, mkiwa na kiburi na majivuno.»
150Basi ogopeni adhabu ya Mwenyezi Mungu na mkubali ushauri wangu
151na msiandame amri ya wenye kuzidhulumu nafsi zao, waliokolea katika kumuasi Mwenyezi Mungu
152waliozoea kufanya uharibifu kwenye ardhi, uharibifu usiotengenezeka
153Watu wa Thamūd walimwambia Nabii wao Ṣāliḥ, «Wewe hukuwa isipokuwa ni miongoni mwa wale waliofanyiwa uganga wa uchawi mwingi, mpaka uchawi ukaathiri akili yako
154Hukuwa wewe isipokuwa ni mmoja wa wanadamu unaofanana na sisi katika ubinadamu, basi vipi utakuwa tafauti na sisi kwa utume? Basi leta hoja wazi inayoonyesha kuwa utume wako umethibiti, iwapo wewe ni mkweli katika madai yako kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza kwetu.»
155Ṣāliḥ akasema kuwaambia- na hapo alikuwa amewaletea ngamia ambaye Mwenyezi Mungu alimtolea kwenye jiwe-, «Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu. Yeye ana hisa ya maji siku maalumu, na nyinyi mna hisa ya maji kwa siku nyingine. Haifai kwenu nyinyi kunywa siku ile ambayo ni hisa yake, na yeye hatakunywa siku ambayo ni hisa yenu
156Na msimguse kwa kitu chochote cha kumdhuru, kama kipigo au mauaji au mfano wake, kwani mkifanya hivyo, Mwenyezi Mungu Atawaangamiza nyinyi kwa adhabu ya Siku ambayo shida yake ni kubwa kwa sababu ya papatiko litakalotukia Siku hiyo na shida
157Basi wakamchinja ngamia, wakawa ni wenye kujuta kwa walilolifanya walipokuwa na uhakika kuwa watashukiwa na adhabu, na majuto yao yasiwafae kitu
158Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ikawashukia, ile ambayo Ṣāliḥ, amani imshukiye, aliwaahidi nayo, na ikawaangamiza. Kwa hakika, katika kuwaangamiza watu wa Thamūd pana mazingatio kwa mwenye kuuzingatia mwisho huu; na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini
159Na kwa hakika Mola wako Ndiye Mshindi, Mwenye kutendesha nguvu, Mwenye kuwatesa maadui Wake, Mwenye huruma kwa walioamini miongoni mwa viumbe Wake
160watu wa Lūṭ waliukanusha utume wake, wakawa kwa hilo ni wakanushaji wa Mitume waliosalia, kwa kuwa lile walilolileta la kumpwekesha Mwenyezi Mungu na misingi ya Sheria ni moja
161Pindi ndugu yao Lūṭ alipowaambia, «Je, hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu
162Mimi ni mjumbe kutoka kwa Mola wenu aliye muaminifu juu ya utekelezaji wa ujumbe Wake kwenu
163Basi jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa kumkanusha kwenu mjumbe Wake, na nifuateni mimi katika yale ninayowalingania
164Na siwaombi malipo yoyote juu ya ulinganizi wangu wa kuwaongoza, malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote
165«Mnawaingilia binadamu wanaume
166na mnawaacha wake zenu ambao Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi ili mstarehe na mzaane? Lakini nyinyi ni watu, kwa uasi huu, wenye kuyakiuka yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaruhusu ya halali na kuyaendea ya haramu.»
167Watu wa Lūṭ wakasema, «Usipoacha, ewe Lūṭ, kutukataza kuwajia wanaume na kukichafua kitendo hicho (cha kuwajia wanaume), utakuwa ni miongoni mwa wenye kufukuzwa kutoka miji yetu.»
168Lūṭ akasema kuwaambia wao, «Mimi ni miongoni mwa wale wanaokichukia sana kitendo chenu mnachokifanya cha kuwajia wanaume.»
169Kisha Lūṭ akamuomba Mola wake, alipokata tamaa kuwa watamsikiliza, alisema, «Mola wangu! Niokoe mimi na uwaokoe jamaa zangu na kile wanachokifanya watu wangu cha uasi huu mchafu na (utuokoe na) adhabu yako itakayowapata.»
170Basi tukamuokoa yeye na watu wa nyumbani kwake na wale wote walioukubali ulinganizi wake
171isipokuwa mkongwe miongoni mwa watu wa nyumbani kwake, naye ni mke wake ambaye hakushirikiana na wao katika kuamini, hivyo basi akawa ni mwenye kusalia kwenye adhabu na maangamivu
172Kisha tukawaangamiza wasiokuwa wao, miongoni mwa makafiri, kuwaangamiza kukubwa
173na tukawateremshia wao mawe kutoka juu kama mvua yakawaangamiza. Ilikuwa mvua mbaya sana ya wale walioonywa na Mitume wao na wasiwakubalie. Kwa hakika, wao wameteremshiwa aina mabaya zaidi za maangamivu na uvunjaji
174Kwa hakika, katika mateso hayo yaliyowateremkia watu wa Lūṭ pana mazingatio na mawaidha ya kuwafanya wenye kukanusha wawaidhike. Na wengi wao hawakuwa ni wenye kuamini
175Na kwa kweli Mola wako Ndiye Mshindi Mwenye nguvu ya kuweza kuwashurutisha wakanushaji, Mwenye huruma kwa waja Wake wema
176Walimkanusha watu wa nchi yenye miti iliyoshikana Mtume wao Shu’ayb kuhusu utume wake, na kwa hivyo waliukua wamekanusha jumbe zote za Mitume
177Alipowaambia wao Shu’ayb, «Je, hamuogopi kuwa Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa ushirikina wenu na kufanya kwenu matendo ya uasi
178Mimi nimetumilizwa kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu niwaongoe, ni mtunzi wa kile alichoniletea mimi Mwenyezi Mungu cha wahyi wa utume
179Basi yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu na mkifuate kile ninachowaitia cha uongofu wa Mwenyezi Mungu mupate kuongoka
180Na sitaki kwenu, kwa kule kuwalingania kwangu kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, malipo yoyote. Malipo yangu hayako isipokuwa kwa Mola wa viumbe wote.”
181Shu’ayb akaendelea kuwaambia- na walikuwa wakipunguza vipimo na mizani-, «Watimizieni watu vipimo kwa kuwakamilishia, na msiwe ni kati ya wale wanaowapunja watu haki zao
182na mpime kwa mizani ya uadilifu iliyolingana sawa
183na msiwapunje watu chochote katika haki zao kwenye vipimo au mizani au vinginevyo, na msizidishe uharibifu katika ardhi kwa kufanya ushirikina, kuua, kunyang’anya, kuwatisha watu na kutekeleza vitendo vya uasi
184«Na jihadharini na mateso ya Mwenyezi Mungu Aliyewaumba na Akawaumba watu wa mataifa yaliyowatangulia.»
185Wakasema, «Ukweli ni kwamba wewe, ewe Shu’ayb, ni miongoni mwa wale waliopatwa na uchawi ukawashika sana ukawaondoa akili zao
186Na wewe hukuwa isipokuwa ni mfano wetu sisi katika ubinadamu, basi vipi utahusika peke yako kwa utume bila ya sisi? Na kwa kweli, dhana yetu kubwa kuhusu wewe ni kuwa wewe ni miongoni mwa warongo katika kile unachokidai cha utume
187Iwapo wewe ni mkweli katika madai yako ya utume, basi muombe Mwenyezi Mungu Atuangushie vipande vya adhabu kutoka mbinguni vitumalize.»
188Shu’ayb akawaambia wao, «Mola wangu Anayajua zaidi yale mnayoyafanya ya ushirikina na uasi na mateso mnayostahili.»
189Wakaendelea kumkanusha, likawapata wao joto kali, wakawa wanatafuta mahali pa hifadhi ili wajifinike. Kikawafinika kiwingu, kikawapatia ubaridi na upepo laini, na walipokusanyika chini yake, moto uliwawakia na ukawachoma, basi hapo yakawa maangamivu yao wote katika siku yenye kitisho kikali
190Hakika katika mateso hayo yaliyowashukia kuna ushahidi wazi juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu katika kuwapatiliza wakanushaji kwa adhabu na kuna mazingatio kwa mwenye kuzingatia. Na hawakuwa wengi wao ni wenye kuamini na kuwaidhika kwa hayo
191Na kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Yeye Aliye Mshindi katika kuwatesa Kwake wale Anaowatesa miongoni mwa maadui Wake, Ndiye Anayewarehemu waja Wake wanaompwekesha
192Na kwa hakika, hii Qur’ani ambayo ndani yake zimetajwa habari hizi za kweli imeteremshwa na Muumba viumbe na Mmiliki wa mambo yote
193Jibrili muaminifu ameshuka nayo
194akakusomea mpaka ukaikusanya moyoni mwako, kwa kuihifadhi na kuielewa, upate kuwa ni mmoja wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu wenye kuwafanya watu wao waogope mateso ya Mwenyezi Mungu, upate kuwaonya, kwa Teremsho hili, binadamu na majini wote
195Ameshuka nayo Jibrili kwako kwa lugha ya Kiarabu yenye maana yaliyo wazi, yenye ushahidi unaoonekena, ikikusanya kile wanachokihitajia cha kutengeneza mambo ya Dini yao na dunia yao
196Na kwa hakika, utajo wa hii Qur’ani umethibitishwa katika Vitabu vya Manabii waliotangulia, vimeibashiri na kukubali kuwa ni ya kweli
197Je, haiwatoshi hawa kuwa ni ushahidi kwamba wewe ni mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba Qur’ani ni kweli kuwa wasomi wa Wana wa Isrāīl wana ujuzi wa usahihi wa hilo na wale walioamini miongoni mwao kama ‘Abdullāh bin Sallām
198Na lau tungaliiteremsha Qur’ani kwa baadhi ya wale wasiozungumza lugha ya Kiarabu
199wakawasomea makafiri wa Kikureshi kisomo cha Kiarabu kilicho sawa, wangaliikanusha pia na wangalizua sababu ya ukanushaji wao
200Hivyo ndivyo tulivyotia ndani ya nyoyo za wahalifu kuikanusha Qur’ani na hilo likawa limejikita ndani ya hizo nyoyo
201na hii ikawa ni sababu ya udhalimu wao na uhalifu wao. Basi hapana njia ya wao kubadilika kwa kuyaacha waliyonayo ya kuikanusha Qur’ani mpaka waishuhudie adhabu kali walioahidiwa
202Hapo adhabu iwashukie ghafla na hali wao hawajui kuja kwake kabla ya hapo
203na hapo waseme, watakaposhtushwa nayo, kwa majuto ya Imani iliyotupita tukaikosa, «Je, sisi ni wenye kupatiwa nafasi na kucheleweshwa tupate kutubia kwa Mwenyezi Mungu ushirikina wetu na tuyapatilize yaliyotupita?»
204Je, hawa wamedanganyika na kule kuwapa muhula kwangu ndipo wakawa wanataka kuteremka adhabu kwa haraka juu yao kutoka mbinguni
205Je, umejua, ewe Mtume, lau tungaliwastarehesha kwa uhai wa miaka mingi kwa kuwacheleweshea muda wao wa kuishi
206kisha iwashukie adhabu ilioahidiwa
207Hakutawafaa kitu kule kustarehe kwao kwa umri mrefu na maisha mazuri wasipotubia kutokana na ushirikina wao. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuwashukia hivi karibuni (ulimwenguni) au baadaye (huko Akhera)
208Na hatukuuangamiza mji wowote, miongoni mwa miji katika mataifa yote, isipokuwa baada ya kuwatumiliza Mitume kwao wawaonye
209ili wawe ni makumbusho kwao na uzindushi wa yale yenye uokofu kwao. Na hatukuwa ni wenye kudhulumu kwa kuwaadhibu watu kabla ya kuwapelekea Mtume
210Na Qur’ani hawakuiteremsha mashetani kwa Muhammad, kama wanavyodai makafiri
211na hilo halifai kutoka kwao na wala hawaliwezi
212kwa kuwa wao ni wenye kuzuiliwa kuisikiliza Qur’ani kutoka mbinguni, ni wenye kupigwa na vimondo
213Hivyo basi usiabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, muabudiwa yoyote asiyekuwa Yeye, ufanyapo hivyo utateremkiwa na adhabu ile iliyowashukia hawa walioabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu, asiyekuwa Yeye
214Na watahadharishe, ewe Muhammad, watu wako wa karibu, ukianzia na wale walio karibu na wewe zaidi, isije adhabu yetu ikawashukia
215Na uwe laini wa mwenendo na maneno, kwa unyenyekevu na huruma, kwa yule ambaye imekufunukia kutoka kwake kuitika mwito wako
216Basi wakienda kinyume na amri yako na wasikufuate, jiepushe na vitendo vyao na yale waliyonayo ya ushirikina na upotevu
217Na Umuachie jambo lako Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye wala wa kumlazimisha, Mwenye kurehemu Ambaye Hawaachi wenye kumtegemea
218Na Ambaye Anakuona unaposimama kuswali ukiwa peke yako ndani ya usiku
219Na Anaona vile unavyogeuka, pamoja na wenye kumsujudia katika Swala zao wakiwa na wewe, ukiwa katika hali ya kusimama, kurukuu na kusujudu na kuketi
220Hakika Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayesikia kusoma kwako na kumtaja kwako, Ndiye Anayejua nia yako na matendo yako
221Je, niwapashe habari, enyi watu, ni nani ambaye mashetani wanamshukia
222Wanamshukia kila mwingi wa urongo, mwingi wa madhambi miongoni mwa makuhani
223Mashetani wanasikiliza kwa kuiba, wanayanyakuwa maneno kutoka sehemu za juu wakawatupia makuhani na wale wanaokuwa na mwenendo wao miongoni mwa watu wenye matendo mabaya. Na wengi wa hawa ni warongo, kwani mmoja wao husema kweli katika neno moja na akaongeza juu yake maneno mia moja ya urongo
224Na washairi, mashairi yao yanasimama juu ya ubatilifu na urongo, na wanafuatana na wao wapotevu waliopotoka kama wao
225Kwani huoni, ewe Nabii, kwamba wao wanaenda kama mtu aliyekosa mwelekeo, wanavama ndani ya kila aina ya fani za urongo, uzushi, uvunjaji heshima, kutukana nasaba na kuwataja vibaya wanawake waliojihifadhi
226na kwamba wao wanayasema wasiyoyatenda, wanapita mipaka katika kuwasifu watu wa ubatilifu na wanawatia kasoro watu wa haki
227Mwenyezi Mungu amewavua, kati ya hao washairi, wale washairi walioongoka kwa kuamini na kufanya matendo mema, na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi, wakatunga mashairi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kumsifu Yeye, Mwenye utajo mtukufu, na kumtetea Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasema maneno ya busara yenye mawaidha na adabu nzuri, na wakaunusuru Uislamu wakawa wanamtukana anayeutukana au anayemtukana Mtume wake kwa kuwarudi washairi makafiri. Na watajua wale waliozidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na matendo ya uasi, wakawadhulumu wasiokuwa wao kwa kuwanyima haki zao au kuwafanyia uadui au tuhuma za urongo, ni marejeo gani ya shari na maangamivu watakayorejea. Kwa kweli, hayo ni mageuko mabaya. Tunamuomba Mwenyezi Mungu salama na afya
chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr
WEBREATH · 11:11
«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7
Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.
WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath