Uislamu
nyuma

23. Al-Muminoon

1Kwa hakika wamefaulu wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kuzitumia sheria Zake

2Wale ambao miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao ni wanyenyekevu kwenye Swala zao, nyoyo zinajishughulisha na hiyo Swala tu na viungo vyao vimetulia kwayo

3Na wale ambao wanaacha kila lisilo na wema ndani yake, la maneno na la vitendo

4Na wale ambao wanazitakasa nafsi zao na mali zao kwa kutoa Zaka za aina mbalimbali za mali zao

5Na wale ambao wanazihifadhi tupu zao kwa kuziepusha na mambo Al;iyoyafanya haramu Mwenyezi Mungun ya uzinifu, ulawiti na machafu mengine

6Isipokuwa kwa wake zao au wajakazi waliomilikiwa na mikono yao ya kulia. Hao, Waumini hawana lawama wala makosa kuwaingilia na kujistarehesha nao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewahalalishia

7Basi mwenye kutaka kujistarehesha na asiyekuwa mkewe au mjakazi wake, huyo ni miongoni mwa wenye kuikiuka halali na kuijia haramu na atakuwa amejiorodhesha nafsi yake kwenye mateso ya Mwenyezi Mungu na hasira Zake

8Na wale ambao wanavitunza vitu vyote walivyoaminiwa nazo na wanatekeleza ahadi zao zote

9Na wale ambao daima wanazitekeleza Swala zao kwa nyakati zake na kwa namana iliyowekwa na Sheria iliyokuja kutoka kwa Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye

10Hao ndio Waumini wenye kuirithi Pepo

11Ambao watairithi Pepo ya juu kabisa na ya kati na kati, nayo ndiyo yenye mashukio bora zaidi kuliko zote, wao humo watakaa milele, neema zao hazitakatika wala hazitaondoka

12Na kwa hakika tulimuumba Ādam kutokana na udongo uliochukuliwa kutoka ardhi yote

13Kisha tukawaumba watoto wake wakiwa ni wenye kuzaana kutokana na tone la maji: nalo ni manii ya wanaume, yanatoka kwenye migongo yao na yanatulia ndani ya zao za wanawake

14Kisha tukaliumba hilo tone kwa kuligeuza kulifanya pande la damu iliyo nyekundu, kisha tukaliumba pande la damu kwa kuligeuza kulifanya kinofu cha nyama kadiri ya kutafunika baada ya siku arubaini, na tukakiumba kinofu cha nyama kilicho laini kwa kukigeuza kukifanya mifupa, na tukaivisha nyama ile mifupa, kisha tukamfanya ni kiumbe kingine kwa kuvuvia roho ndani yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kheri nyingi Ambaye Ametengeneza umbo la kila kitu

15Kisha nyinyi, enyi binadamu, baada ya vipindi vya maisha na umri kukoma, mtakufa

16Kisha nyinyi, baada ya kufa na dunia kumalizika, mtafufuliwa mkiwa hai kutoka makaburini mwenu muhesabiwe na mlipwe

17Kwa hakika tuliziumba juu yenu mbingu saba, moja juu ya nyingine, na hatukuwa tumeghafilika na viumbe, hatughafiliki na kiumbe wala hatumsahau

18Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kadiri ya mahitaji ya viumbe, na tumeifanya ardhi kuwa ni mahali pa kutulia haya maji, na sisi niwaweza wa kuyaondoa maji haya yaliyotulia. Katika haya pana kitisho na onyo kwa wenye udhalimu

19Tukawafanyia kwa maji haya mashamba ya mitende na mizabibu, mukawa nayo nyinyi kutokana na mashamba hayo matunda ya aina nyingi na sampuli mbalimbali, na katika hayo munakula

20Na tukawatolea nyinyi kwa maji hayo mizaituni ambayo inatoka kandokando ya jabali la Tūr Ṣīnā’ ambao unakamuliwa mafuta ya kujipaka na kutumia kwa chakula

21Na nyinyi, enyi watu, muna mazingatio katika ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo ya kulizingatia namna ya kuumbwa kwao. Tunawanywesha maziwa yanayotoka matumboni mwao. Na munayo nyinyi kutokana nao manufaa mengine mengi kama sufi na ngozi na mfano wa hivyo, na miongoni mwao mnakula

22Na juu ya ngamia na majahazi, katika nchi kavu na baharini munabebwa

23Kwa hakika, tulimtumiliza Nūḥ kwa watu wake kuwalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, (alipokwenda) akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu peke Yake, nyinyi hamuna muabudiwa yoyote isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, basi mtakasieni ibada. Kwani nyinyi hamuiogopi adhabu yake?»

24Basi wale waheshimiwa wa watu wake walimkanusha na wakasema kuwaambia watu wa kawaida wao, «Yeye ni mwanadamu kama nyinyi, hana ubora wowote wa kutafautiana na nyinyi, na hataki kwa maneno yake isipokuwa uongozi na utukufu juu yenu, na lau Mwenyezi Mungu Alitaka kutuletea mtume, Angalimtuma Malaika kwetu, hatujasikia mfano wa hili kwa watu waliotutangulia miongoni mwa mababa na mababu. Na huyu Nūh

25hakuwa isipokuwa ni mwanamume aliyeshikwa na wazimu, basi ngojeeni mpaka atakapopata fahamu auache ulinganizi wake au afe mupumzike na yeye.»

26Nūḥ akasema, «Mola wangu! Niokoe na watu wangu kwa sababu ya kunikanusha mimi kwa yale niliyowafikishia ya ujumbe wako.»

27Hapo tukamletea wahyi na kumwambia, «Tengeneza jahazi chini ya uangalizi wetu na amri yetu kwako na usaidizi wetu, na wewe uko kwenye utunzi wetu na hifadhi yetu. Basi amri yetu itakapokuja ya kuwaadhibu watu wako kwa kuwazamisha, na mafuriko yakaanza, na maji yakatembuka kwa nguvu kwenye tanuri, napo ni mahali pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja kwa adhabu, hapo basi watie ndani ya jahazi, kati ya kila kilicho hai, kiume na kike, ili kizazi kisalie. Na uwatie watu wako pia, isipokuwa yule aliyestahili kuadhibiwa kwa ukafiri wake, kama mke wako na mwano wa kiume, na usiniombe kuokolewa watu wako waliodhulumu, kwani wao hapana budi ni wenye kuzamishwa. Na katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya jicho kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kama inavyonasibiana na Yeye, Aliyetukuka, bila kufananisha wala kulifanya liko namna gani

28‘’Basi ukiwa juu ya jahazi na ukatulia humo wewe na walio pamoja na wewe, mukiwa mumesalimika na kuzama, sema, ‘Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuokoa na watu makafiri.’»

29Na useme, «Mola wangu! Nifaniye wepesi uteremkaji uliobarikiwa wenye amani, na wewe ndiye bora wa wenye kuteremsha.» Katika hili pana mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, kwa waja Wake wasome dua hii wateremkapo mahali

30Kwa hakika, katika kuwaokoa Waumini na kuwaangamiza makafiri, pana dalili wazi zakuonesha ukweli wa Mitume wa Mwenyezi Mungu katika yale waliokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sisi ni wenye kuwapa mtihani watu kwa kuwapelekea Mitume kwao kabla mateso hayajawashukia

31Kisha tukawaleta baada ya watu wa Nūḥ kizazi kingine, nacho ni kile cha watu wa kabila la ‘Ād

32Tukampeleka kwao Mtume miongoni mwao, naye ni Hūd, amani imshukiye, akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamuna muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Je, hamuogopi mateso Yake mtakapomuabudu asiyekuwa Yeye?»

33Watukufu na viongozi waliomkufuru Mwenyezi Mungu miongoni mwa watu wake na waliokataa kuwa kuna maisha ya Akhera na zikawafanya wakiuke mipaka zile neema walizoneemeshwa ulimwenguni za maisha ya anasa za kupindukia, «Huyu anayewaita mumpwekeshe Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, si lolote isipokuwa ni mwanadamu kama nyinyi, anakula chakula cha aina mnachokula nyinyi, na anakunywa aina ya kinywaji mnachokunywa

34«Na lau mtamfuata binadamu kama nyinyi, basi nyinyi mtakuwa wakati huo ni wenye kupata hasara kawa kuwaacha waungu wenu na kumfuata yeye

35«Vipi mtayaamini yale anayowaahidi kwamba nyinyi mkifa na mkawa mchanga na mifupa iliyovunjika vipande-vipande, kuwa mtatolewa kutoka kwenye makaburi yenu mkiwa hai

36«Kwa hakika, liko mbali sana hilo mnaloahidiwa, enyi watu, la kwamba nyinyi mtatolewa makaburini mwenu mkiwa hai baada ya kufa kwenu

37«Maisha yetu ni ya hapa duniani tu, wazazi wanakufa na watoto wanaishi. Na sisi si wenye kutolewa tukiwa hai mara nyingine

38«Na huyu, Anayewalingania kwenye Imani, hakuwa isipokuwa ni mtu amemzulia Mwenyezi Mungu urongo. Na sisi si wenye kuyaamini anayoyasema.»

39Hapo Mtume wao Alimuomba Mola wake akisema, «Ewe Mola wangu! Ninusuru juu yao kwa kuwa wamenikanusha.»

40Mwenyezi Mungu Akasema Akiyakubali maombi yake, «Kwa muda mchache watakuwa ni wenye kujuta.» Yaani, baada ya kipindi cha muda mchache watakuwa na majuto hao wakanushaji.»

41Hawakupitiwa na muda, uliwajia wao ukelele mkali pamoja na upepo ambao kwa upepo huo Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza, wakafa wote na wakawa ni kama takataka za mtiririko wa maji zinazoelea juu ya maji. Basi maangamivu ni ya hawa madhalimu, na kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwao. Kwa hivyo, na wajihadhari wenye kusikia, wasije wakawakanusha Mitume wao, ikawashukia wao adhabu ilyowashukia waliowatangulia

42Kisha tukawaleta, baada ya hawa waliokanusha, ummah na viumbe wengine, kama watu wa Lūṭ, Shu'ayb, Ayyūb na Yūnus, rehema za Mwenyezi Mungu na amani Yake ziwashukie

43Hautangulii ummah wowote, miongoni mwa ummah hawa wanaokanusha Mitume wao, muda uliowekewa kuangamia kwake, wala hauchelewi

44Kisha tukawapeleka Mitume wetu waende kwa ummah hao, wakifuatana: hawa baada wengine. Na kila Mtume akiwalingania watu wake, wanamkanusha. Basi tukawafuatisha, kundi baada ya kundi, kwa kuwaangamiza na kuwamaliza, na hakuna kilichosalia isipokuwa ni habari za kuangamia kwao.Na tukazifanya habari hizo ni maneno ya kuzungumzwa na watu waliokuja baada yao, wakizichukuwa kuwa ni mazingatio. Basi maangamivu na kuepushwa na kila kheri ni kwa watu wasiowaamini Mitume wala kuwatii

45Kisha tukampeleka Mūsā na ndugu yake Hārūn kwa alama zetu tisa, nazo ni fimbo, mkono, nzige, chawa, vyura, damu, mafuriko, shida za maisha na upungufu wa matunda, zikiwa ushahidi uliyo wazi wenye kuzishinda nyoyo, zipate kulainika kwa alama hizo nyoyo zaWaumini, na isimame hoja juu ya washindani. Tuliwapeleka wao wawili

46kwa Fir'awn, hakimu wa Misri, na watukufu wa watu wake ambao walifanya kiburi wakakataa kumuamini Mūsā na ndugu yake. Na wao walikuwa ni watu wanaojiona bora kuliko watu wengine na walikuwa wakiwanyanyasa kwa kuwadhulumu

47Wakasema, «Je, tuwaamini watu wawili kama sisi, na jamaa zao Wana wa Isrāīl wako chini ya amri yetu, wanatutii na wanajidhalilisha kwetu.?»

48Basi wakawakanusha katika yale waliyokuja nayo, wakawa ni wenye kuangamizwa kwa kuzamishwa baharini

49Hakika tulimletea Mūsā Taurati, ili watu wake wajiongoze nayo kwenye haki

50Na tulimjaalia Īsā mwana wa Maryam na mamake ni alama yenye kuonesha uweza wetu, kwani tulimuumba bila ya baba, na tulimfanyia makao kwenye ardhi iliyopo mahali pa juu palipolingana ili apate utulivu juu yake, penye urutuba na maji yapitayo yanayoonekana waziwazi kwa macho

51Enyi Mitume! Kuleni riziki ya halali na fanyeni matendo mema, kwani mimi kwa mnayoyafanya ni mjuzi, hakuna kitu chochote chenye kufichika kwangu katika matendo yenu. Wanaohutubiwa katika aya hii ni Mitume wote kwa jumla, amani iwashukie, na wafuasi wao. Na katika aya pana dalili kwamba kula halali inasaidia kufanya matendo mema na kwamba mwisho wa haramu ni mbaya na miongoni mwa ubaya wake ni kurudishwa dua kwa kutokubaliwa

52Na kwa hakika Dini yenu, enyi Mitume, ni Dini moja, nayo ni Uislamu, na mimi ni Mola wenu niogopeni kwa kufuata maamrisho yangu na kujiepusha na makatazo yangu

53Na wafuasi walipambanukana katika dini wakawa makundi na mapote, wakaifanya dini yao kuwa dini nyingi baada ya kuamrishwa wajikusanye pamoja. Kila kundi linajigamba kwa maoni yake, linadai kuwa kundi hilo liko kwenye haki na lingine liko kwenye batili. Katika haya pana onyo la kujiweka kwenye makundi na kupambanukana katika Dini

54Basi waache , ewe Mtume, kwenye upotevu wao na ujinga wao wa kutoijua haki hadi pale adhabu itakapowashukia

55Kwani wanadhani hawa makafiri kwamba yale tunayowapa ya mali na watoto ulimwenguni ni mazuri waliyoharakishiwa na kwamba wao wanastahiki hayo

56Hakika tunawaharakishia haya mazuri kwa kuwatahini na kwa kuwavuta kidogo kidogo, lakini wao hawalihisi hilo

57Hakika wale ambao kwa kumcha Mola wao wanayaogopa na kujitahadhari na yale Aliyowaogopesha nayo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka

58Na wale ambao wao wanaziamini aya za Mwenyezi Mungu katika Qur’ani na wanazitumia

59Na wale ambao wao wanaitakasa ibada kwa Mwenyezi Mungu , Peke Yake, na hawamshirikishi na Yeye mwingine asiyekuwa Yeye

60Na wale wanaojibidiisha kufanya matendo ya kheri na wema, mioyo yao ina kicho cha kuogopa yasikubaliwe matendo yao na yasiwaokoe na adhabu ya Mola wao warejeapo Kwake kwa kuhesabiwa

61Hao wanaojibidiisha kutii, dasturi yao ni kukimbilia kufanya kila kitendo chema, na wao kwa kuyaendea mambo mema ni wenye kutangulia

62Hatumlazimishi mja yoyote miongoni mwa waja wetu isipokuwa kile kinachomkunjukia kukifanya, na matendo yao yamesajiliwa kwetu ndani ya Kitabu cha kudhibiti matendo, ambacho Malaika watakiinua, kitakachosema ukweli juu yao, na hakuna yoyote kati yao Atakayedhulumiwa

63Lakini nyoyo za makafiri ziko kwenye upotevu uliowafinika, zimejiepusha na Qur’ani na yaliyomo ndani yake. Na wao, pamoja na ushirikina wao, wana matendo mabaya, Mwenyezi Mungu Anawapa muhula wayafanye, ili ziwapate wao hasira za Mwenyezi Mungu na mateso Yake

64Mpaka tutakapowashika wenye gogi na kiburi miongoni mwao kwa adhabu yetu, hapo ndipo watainua sauti zao wakinyenyekea na wakiomba waokolewe

65Na hapo waambiwe, «Msipige kelele wala msiombe kuokolewa leo! Nyinyi hamuwezi kuziokoa nafsi zenu, na hakuna yoyote atakayewaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu

66«Zilikuwa aya za Qur’ani zikisomwa kwenu, ili mupate kuziamini, na mlikuwa mnazikimbia hamtaki kuzisikia na kuzikubali na kuzitumia, kama anavyofanya mwenye kurudi nyuma kwa kule kurudi kwake nyuma

67«Mnalifanya hilo na huku mnawaonesha watu kiburi pasi na haki kwa sababu ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu. Mnasema, ‘Sisi ni watu wa Nyumba hiyo, hatushindwi tukiwa hapo,’ na mnakesha mkiwa kando-kando yake kwa maneno maovu.»

68Kwani hawayafikirii yaliyomo ndani ya Qur’ani wakapata kujua ukweli wake au limewazuia wao kuamini kwa kuwa wamejiwa na Mtume na kitabu ambacho mfano wake hakikuwajia baba zao wa mwanzo, wakakikanusha kwa ajili hiyo na wakakipa mgongo

69Au limewazuia wao kuifuata haki kwa kuwa Mtume wao, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hajulikani kwao na kwa hivyo wanamkataa

70Au wanamdhania kuwa ni mwendawazimu? Kwa hakika wamedanganya. Ukweli ni kuwa amewajia na Qur’ani, upwekeshaji Mwenyezi Mungu na dini ya kweli. Na wengi wao wanaichukia haki kwa uhasidi na uadui

71Lau kama Mwenyezi Mungu Angaliwawekea sheria inayolingana na mapendeleo yao, zingaliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo humo. Bali tumewaletea yale ambayo ndani yake muna alama za nguvu yao na utukufu wao, nayo ni Qur’ani, na wao wanaipa mgongo

72Au limewazuia wao kukuamini kwa kuwa wewe, ewe Mtume, unawaomba malipo juu ya ulinganizi wako kwao, hivyo basi wakafanya ubahili? Hukufanya hivyo, kwa kuwa zile thawabu zilizoko kwa Mwenyezi Mungu na vipewa ni bora zaidi. Na Yeye ni bora wa wanaoruzuku, hakuna awezaye kuruzuku kama Yeye Anavyoruzuku, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake

73Kwa hakika wewe, ewe Mtume, unawalingania watu wako na wengineo kwenye Dini iliyolingana sawa, nayo ni Dini ya Uislamu

74Na kwa hakika, wale ambao hawaamini kufufuliwa na kuhesabiwa wala hawayafanyii kazi hayo mawili, basi hao wamepotoka kando ya njia ya Dini iliyonyoka, nayo ni dini ya Uislamu

75Na lau tungaliwahurumia na tukawaaondolea ukame na njaa, wangaliendelea kwenye ukafiri na ushindani, wakiwa katika hali ya kuduwaa na kukosa muelekeo

76Na kwa hakika, tuliwajaribu wao kwa kuwaonja kwa aina mbalimbali za mikasa, pamoja na hivyo wasimnyenyekee Mola wao na wasimuombe kwa unynyekevu wakati wa kushukiwa na hiyo mikasa

77Mpaka tulipowafungulia juu yao mlango wa adhabu kali huko Akhera, wakitahamaki wamo ndani yake, wamekata tamaa kupata kheri yoyote, wamechanganyikiwa hawajui wafanye nini

78Na yeye Ndiye Aliyewaumbia masikizi ya kuvisikia venye kusikika, na macho ya kuviona venye kuonekana, na nyoyo ili muelewe. Pamoja na hayo, shukrani zenu kwa hizi neema za mfululizo juu yenu bado ni chache hata hazitajiki

79Na yeye Ndiye Aliyewaumba watu wote katika ardhi, na Kwake Yeye mtakusanywa baada ya kufa kwenu, na hapo Atawalipa kwa mliyoyatenda, mema au maovu

80Na Yeye , Peke Yake, Ndiye Anayehuisha kutoka katia hali ya kutokuweko, na Ndiye Atakayefisha baada ya uhai. Na ni kwake Yeye kufuatana usiku na mchana na pia kupishana. Basi hamuuweki akilini mwenu uweza Wake na upweke Wake

81Lakini makafiri hawakuamini kuwa kuna kufufuliwa, lakini waliyakariri maneno ya wakale wao wakanushaji

82walisema «Ati tutakapokufa na miili yetu ikatangamana na mchanga wa ardhi pamoja na mifupa yetu tutafufuliwa mara nyingine? Hili haliwi wala haliingii akilini.»

83Yameshasemwa maneno haya kuambiwa wazee wetu kitambo, kama vile unavyotuambia, ewe Muhammad, hatukuyaona kuwa yana uhakika. Hayakuwa haya isipokuwa ni porojo za watu wa kale

84Waambie, «Ni ya nani Ardhi hii na walio ndani yake iwapo muna ujuzi?»

85Watakubali kwa lazima kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, Yeye Ndiye Muumba wake na Ndiye Mwenye kuimiliki. Waambie, «Je, haliwi hilo kwenu ni lenye kuwafanya mukumbuke kuwa Yeye ni Muweza wa kuwafufua wafu na kuwarudishia uhai?»

86Sema, «Ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arsh iliyo kubwa, ambayo ndiyo kiumbe kikubwa kabisa na kilichoko juu kabisa?»

87Watasema kwa lazima kuwa hizo ni milki ya Mwenyezi Mungu. Basi waambie, «Mbona hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu mnapomuabudu asiyekuwa Yeye?»

88Sema, «Ni nani mmiliki wa kila kitu? Na ni nani Ambaye mkononi Mwake kuna hazina za kila kitu? Na ni nani Anayempa himaya mwenye kutaka himaya Yake, ambapo hakuna anayeweza kumhami na kumlinda yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuangamiza wala hakuna anayekinga shari Aliyoikadiria Mwenyezi Mungu, iwapo mnalijua hilo?»

89Watajibu kuwa hayo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Sema uwaambie, «Vipi zinaondoka akili zenu na mnadanganywa na mnaepushwa njia ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kuyaamini mambo ya kufufuliwa na kurudishiwa uhai?»

90Ilivyo ni kwamba tumewaletea wakanushaji hawa ukweli wa yale tuliyompeleka kwayo Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na kwa hakika wao ni warongo kwenye ushirikina wao na ukanushaji wao kufufuliwa

91Mwenyezi Mungu Hakujifanyia mwana, na hakukuwa pamoja na Yeye muabudiwa mwingine, kwani kama kungalikuwa huko kuna waabudiwa zaidi ya mmoja pamoja na Yeye, basi kila muabudiwa angalijitenga na alivyoviumba na kungalikuwa na ushindani kati yao kama ilivyo kwa watawala wa ulimwnguni. Hapo mpango wa ulimwengu ungaliharibika. Ametakasika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuepukana na sifa wanazompa za kuwa Yeye ana mshirika au mwana

92Yeye, Peke Yake, Ndiye Anayejua yanayofichika kwa viumbe vyake na wanayoyaona. Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameepukana na mshirika ambaye wanadai kuwa Anaye

93Sema, ewe Mtume, «Mola wangu! Unioneshapo kwa hawa washirikina ile adhabu yako uliyowaonya nayo

94basi usiniangamize kwa ile uliyowaangamiza nayo. Na uniokoe na adhabu yako na hasira zako. Usiniweke pamoja na watu washirikina na madhalimu. Bali niingize kwa wale uliokuwa radhi nao.»

95Na kwa hakika sisi tunaweza kukuonesha yale tunayowaahidi ya adhabu

96Pindi wanapokufanyia ubaya maadui zako, ewe Mtume, kwa maneno au vitendo, basi usiwalipe ubaya, lakini uondoshe ubaya wao kwa kuwafanyia wema. Sisi tunayajua mno yale wanayokubandika washirikina ya sifa za ushirikina na kukukanusha, na Atawalipa kwa hayo malipo maovu mno

97Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Najilinda kwako na upotezaji wa Mashetani unaoupelekea kwenye ubatilifu na uharibifu na kuzuia watu wasiifuate haki

98Na ninajilinda kwako, ewe Mola wangu, na kuingiliwa na wao kwenye mambo yangu.»

99Mwenyezi Mungu Anawatolea habari makafiri au waliokiuka mipaka ya amri Yake, Aliyetukuka, walioko kwenye hali ya kusongwa na kifo, mauti yalipowafikia na wakaishuhudia adhabu waliyoandaliwa, hapo huwa akisema kila mmoja wao, «Mola wangu! Nirudisha ulimwenguni

100«Huenda mimi nikayarekebisha yale niliyoyapoteza ya imani na utiifu.» Hatolipata hilo, kwani hatakubaliwa hilo aliloliomba wala hatapewa muhula. Hilo ni neno tu atalisema. Ni neno lisilomnufaisha, na yeye kwa neno hilo si mkweli, kwani lau angalirudishwa ulimwenguni angaliyarudia yale aliyokatazwa. Na Wenye kufa watasalia kwenye kizuizi na kitengo kilichoko kati ya Akhera na duniani mpaka Siku ya kufufuliwa na kukusanywa

101Basi Siku ya Kiyama itakapokuwa, na Malaika anayehusika akavivia kwenye baragumu, na watu wakafufuliwa kutoka makaburini mwao, hapo hakuna kujigamba kwa nasaba kama walivyokuwa wakijigamba nazo duniani wala hapana yoyote atakayemuuliza yoyote

102Basi yule ambaye mema yake yatakuwa mengi na zikawa nzito kwayo mizani za matendo yake Siku ya kuhesabiwa, basi hao ndio wenye kufaulu kupata Pepo

103Na yule ambaye mema yake yatakuwa machache kwenye mizani na maovu yake yatakuwa mengi zaidi, na kubwa zaidi ya hayo maovu ni ushirikina, basi hao ndio ambao wamepita patupu na wakaziangamiza nafsi zao kwenye moto wa Jahanamu, watasalia humo milele

104Moto huo utaunguza nyuso zao, na wao humo watakuwa ni wenye kufinya nyuso, midomo yao imekauka na meno yao yamejitokeza nje

105Wataambiwa, «Je, hamkuwa mkisomewa aya za Qur’ani huko duniani, mkawa mnazikanusha?»

106Wakikubali kuwa Mitume wao waliwapelekea ujumbe na wakawaonya, watasema Siku ya Kiyama, «Mola wetu! Raha zetu, na pia matamanio yetu yalikadiriwa kwetu kwenye ujuzi wako uliotangulia, zilitutawala na kwa hivyo tukawa, katika matendo yetu, ni wenye kupotea na kuwa kando ya njia ya uongofu

107«Mola wetu! Tutoe Motoni na uturudishe duniani. Na huko, tukirudi upotevuni, basi kwa kweli sisi ni madhalimu tunastahili kuadhibiwa.»

108Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Atawaambia, «Kaeni Motoni mkiwa wanyonge wala msiseme na mimi.» Hapo yatakatika maombi yao na matumaini yao

109«Kulikuwa na kundi la waja wangu, nao ni Waumini, wakiomba kwa kusema, ‘Mola wetu! Tumeamini, basi yasitiri madhambi yetu na uturehemu, na wewe ndiye bora wa kurehemu.’

110«Mkajishughulisha kuwacheza shere, mpaka mkasahau kumtaja Mwenyezi Mungu na mkasalia kwenye ukanushaji wenu, na kwa kweli mlikuwa mkiwacheka kwa shere na dharau

111«Mimi nilililipa kundi hili la waja wangu Waumini kwa kuwafanya wafuzu kupata Pepo kwa sababu ya uvumilivu wao juu makero na utiifu kwa Mwenyezi Mungu»

112Na watu waovu wataulizwa wakiwa Motoni, «Mlisalia miaka mingapi ulimwenguni? Na mlipoteza mangapi huko ya kumtii Mwenyezi Mungu?»

113Watasema kwa kituko cha Kisimamo na ukali wa adhabu, «Tulikuwa huko kwa siku moja au sehemu ya siku. Waulize washika hesabu wenye kuhesabu miezi na siku.»

114Hapo Atawaambia «Hamkuketi isipokuwa kipindi kichache, na lau mlivumilia juu ya kumtii Mwenyezi Mungu mungalifaulu kuipata Pepo, kama mungalikuwa na ujuzi wa hilo.» Hivyo ni kwamba kipindi cha kukaa kwao duniani ni kichache sana kulingana na kipindi cha kukaa kwao Motoni milele

115Je, mlidhania, enyi viumbe, ya kwamba sisi tuliwaumba nyinyi mkiwa mumepuuzwa: hakuna maamrisho wala makatazo wala malipo mema wala mateso, na kwamba nyinyi hamtorudishwa kwetu Akhera kwa Hesabu na Malipo

116Ametukuka Mwenyezi Mungu Aliye Mfalme, Anayepelekesha kila kitu, Ambaye Yeye ni Kweli, ahadi Yake ni kweli na onyo Lake ni kweli na kila kitu kutoka Kwake ni kweli. Ametakasika na kuwa Ataumba kitu kwa upuuzi au pasi na maarifa. Hapana mola isipokuwa Yeye, Mola wa ‘Arsh tukufu ambayo ndicho kiumbe kikubwa kuliko vyote

117Na yoyote atakayeabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka, mungu mwingine, asiyekuwa na hoja yoyote juu ya ustahiki wake kuabudiwa. Basi kwa kweli malipo yake juu ya kitendo chake hicho kiovu yako mbele ya Mola wake huko Akhera. Ukweli ni kwamba hakuna kufuzu wala kuokoka kwa makafiri Siku ya Kiyama

118Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Samehe madhambi na urehemu. Na wewe ndiye bora wa anayemrehemu mwenye dhambi, akaikubali toba yake na asimtese kwa dhambi zake

chanzo: Abdullah Muhammad Abu Bakr

WEBREATH · 11:11

«If you are thankful, I will give you more» — Quran 14:7

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath