Zaburi 55
1Ee Mungu, sikiliza maombi yangu, wala usidharau hoja yangu.
2Nisikie na unijibu. Mawazo yangu yananisumbua na nimehangaishwa
3kwa sauti ya adui, kwa kukaziwa macho na waovu, kwa sababu wananiletea mateso juu yangu na kunitukana kwa hasira zao.
4Moyo wangu umejaa uchungu, hofu ya kifo imenishambulia.
5Woga na kutetemeka vimenizunguka, hofu kuu imenigharikisha.
6Nilisema, “Laiti ningekuwa na mbawa za njiwa! Ningeruka niende mbali kupumzika.
7Ningalitorokea mbali sana na kukaa jangwani,
8ningaliharakisha kwenda mahali pa salama, mbali na tufani kali na dhoruba.”
9Ee Bwana, uwatahayarishe waovu na uwachanganyishie semi zao, maana nimeona jeuri na ugomvi mjini.
10Usiku na mchana wanazunguka juu ya kuta zake, uovu na dhuluma vimo ndani yake.
11Nguvu za uharibifu zinatenda kazi mjini, vitisho na uongo haviondoki mitaani mwake.
12Kama aliyenitukana ni adui yangu, ningevumilia, kama mtu mwovu angejiinua dhidi yangu, ningejificha asinione.
13Kumbe ni wewe, mwenzangu, mshiriki na rafiki yangu wa karibu,
14ambaye awali tulifurahia ushirika mzuri, tulipokuwa tukienda na umati hekaluni mwa Mungu.
15Kifo na kiwajie adui zangu ghafula, na washuke kuzimu wangali hai, kwa maana uovu upo ndani yao.
16Lakini ninamwita Mungu, naye Bwana huniokoa.
17Jioni, asubuhi na adhuhuri ninalia kwa huzuni, naye husikia sauti yangu.
18Huniokoa nikawa salama katika vita vilivyopangwa dhidi yangu, ingawa watu wengi hunipinga.
19Mungu anayemiliki milele, atawasikia na kuwaadhibu, watu ambao hawabadilishi njia zao, wala hawana hofu ya Mungu.
20Mwenzangu hushambulia rafiki zake, naye huvunja agano lake.
21Mazungumzo yake ni laini kama siagi, hata hivyo vita vimo moyoni mwake. Maneno yake ni mororo kuliko mafuta, hata hivyo ni upanga mkali uliofutwa.
22Mtwike Bwana fadhaa zako, naye atakutegemeza, hatamwacha kamwe mwenye haki wake aanguke.
23Lakini wewe, Ee Mungu, utawashusha waovu katika shimo la uharibifu. Wenye kiu ya kumwaga damu na wenye hila, hawataishi nusu ya siku zao. Lakini mimi ninakutumaini wewe.
WEBREATH · 11:11
«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25
Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.
WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath