Ukristo
nyuma

Mithali 19

1Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama, kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.

2Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa, wala kufanya haraka na kuikosa njia.

3Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake hata hivyo moyo wake humkasirikia Bwana.

4Mali huleta marafiki wengi, bali rafiki wa mtu maskini humwacha.

5Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo hataachwa huru.

6Wengi hujipendekeza kwa mtawala na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.

7Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote: Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani! Ingawa huwafuata kwa kuwasihi, hawapatikani popote.

8Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe, yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.

9Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa, naye amwagaye uongo ataangamia.

10Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa, itakuwa vibaya kiasi gani kwa mtumwa kuwatawala wakuu.

11Hekima ya mtu humpa uvumilivu, ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.

12Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba, bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.

13Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye, naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.

14Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi, bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.

15Uvivu huleta usingizi mzito, naye mtu mzembe huona njaa.

16Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake, bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.

17Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana, naye atamtuza kwa aliyotenda.

18Mrudi mwanao, kwa maana katika hiyo kuna tumaini, usiwe mshirika katika mauti yake.

19Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake, kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.

20Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho, nawe mwishoni utakuwa na hekima.

21Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu, lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

22Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho, afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

23Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima, kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika, bila kuguswa na shida.

24Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani, lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!

25Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara, mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.

26Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake ni mwana aletaye aibu na fedheha.

27Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho, utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.

28Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.

29Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.

chanzo: Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

WEBREATH · 11:11

«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath