Ukristo
nyuma

Nahumu 1

1Neno alilosema Mungu kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu, Mwelkoshi.

2Bwana ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi; Bwana hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu. Bwana hulipiza kisasi juu ya watesi wake, naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.

3Bwana si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu, Bwana hataacha kuadhibu wenye hatia. Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni vumbi la miguu yake.

4Anakemea bahari na kuikausha, anafanya mito yote kukauka. Bashani na Karmeli zinanyauka na maua ya Lebanoni hukauka.

5Milima hutikisika mbele yake na vilima huyeyuka. Nchi hutetemeka mbele yake, dunia na wote waishio ndani yake.

6Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu? Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali? Ghadhabu yake imemiminwa kama moto, na miamba inapasuka mbele zake.

7Bwana ni Mwema, kimbilio wakati wa taabu. Huwatunza wale wanaomtegemea,

8lakini kwa mafuriko makubwa, ataangamiza Ninawi; atafuatilia adui zake hadi gizani.

9Shauri baya lolote wapangalo dhidi ya Bwana yeye atalikomesha; taabu haitatokea mara ya pili.

10Watasongwa katikati ya miiba na kulewa kwa mvinyo wao. Watateketezwa kama mabua makavu.

11Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja, ambaye anapanga shauri baya dhidi ya Bwana na kushauri uovu.

12Hili ndilo asemalo Bwana: “Ingawa wana muungano nao ni wengi sana, watakatiliwa mbali na kuangamia. Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda, sitakutesa tena.

13Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako, nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”

14Hii ndiyo amri Bwana aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi: “Hutakuwa na wazao watakaoendeleza jina lako. Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kuyeyusha ambazo zipo katika hekalu la miungu yenu. Nitaandaa kaburi lako, kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”

15Tazama, huko juu milimani, miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema, ambaye anatangaza amani! Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako, nawe utimize nadhiri zako. Waovu hawatakuvamia tena; wataangamizwa kabisa.

chanzo: Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

WEBREATH · 11:11

«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath