Ayubu 14
1“Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake ni chache nazo zimejaa taabu.
2Huchanua kama ua kisha hunyauka; huwa kama kivuli kipitacho upesi, wala hadumu.
3Je, unamwekea jicho lako mtu kama huyo? Je, utamleta mbele yako katika hukumu?
4Ni nani awezaye kutoa kitu safi kutoka kitu najisi? Hakuna awezaye!
5Siku za mwanadamu zimewekewa mpaka; umekwisha kutangaza idadi ya miezi yake na kuweka mpaka ambao hawezi kuuvuka.
6Hivyo angalia mbali umwache, hadi awe amekamilisha muda wake kama mtu aliyeajiriwa.
7“Kwa maana lipo tumaini kwa mti; kama ukikatwa utachipuka tena, nayo machipukizi yake mapya hayatakoma.
8Mizizi yake yaweza kuchakaa ardhini na kisiki chake kufa udongoni,
9lakini kwa kupata dalili ya maji utachipua na kutoa machipukizi kama mche.
10Lakini mwanadamu hufa, na huo ndio mwisho wake; hutoa pumzi ya mwisho, naye hayuko tena!
11Kama vile maji yatowekavyo katika bahari, au mkondo wa mto ukaushwavyo na kuwa mkavu,
12ndivyo mwanadamu alalavyo chini asiamke; hadi mbingu zitakapokuwa hazipo tena, wanadamu hawataamka au kuamshwa kutoka kwenye usingizi wao.
13“Laiti kama ungenificha kaburini, na kunisitiri hadi hasira yako ipite! Laiti ungeniwekea wakati, na kisha ukanikumbuka!
14Je, kama mtu akifa, aweza kuishi tena? Siku zote za kazi zangu ngumu nitangojea kufanywa upya kwangu.
15Utaniita nami nitakuitika; utakionea shauku kiumbe ambacho mikono yako ilikiumba.
16Hakika ndipo utakapozihesabu hatua zangu, lakini hutazifuatia dhambi zangu.
17Makosa yangu yatafungiwa kwa lakiri kwenye mfuko, nawe utazifunika dhambi zangu.
18“Lakini kama mlima umomonyokavyo na kufikichika na kama vile mwamba uondolewavyo mahali pake,
19kama maji yamalizavyo mawe, na mafuriko yachukuavyo udongo, ndivyo unavyoharibu tegemeo la mwanadamu.
20Humshinda mara moja kwa daima, naye hutoweka; waibadilisha sura yake na kumwondoa.
21Kama wanawe wakipewa heshima, yeye hafahamu; kama wakidharauliwa, yeye haoni.
22Yeye hasikii kingine isipokuwa maumivu ya mwili wake mwenyewe, naye huomboleza kwa ajili yake mwenyewe.”
WEBREATH · 11:11
«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25
Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.
WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath