Ukristo
nyuma

Yakobo 4

1Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu?

2Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hammwombi Mungu.

3Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

4Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.

5Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?

6Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

7Basi mtiini Mungu. Mpingeni ibilisi, naye atawakimbia.

8Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu ninyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu ninyi wenye nia mbili.

9Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa huzuni.

10Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

11Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu yeyote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria.

12Yuko Mtoa sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu, ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?

13Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.”

14Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka.

15Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.”

16Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu.

17Basi mtu yeyote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

chanzo: Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

WEBREATH · 11:11

«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath