Ukristo
nyuma

Isaya 11

1Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese, kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.

2Roho wa Bwana atakaa juu yake, Roho wa hekima na wa ufahamu, Roho wa shauri na wa uweza, Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana

3naye atafurahia kumcha Bwana. Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake, wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,

4bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji, kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia. Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.

5Haki itakuwa mkanda wake na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.

6Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo, naye chui atalala pamoja na mbuzi, ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja, naye mtoto mdogo atawaongoza.

7Ngʼombe na dubu watalisha pamoja, watoto wao watalala pamoja, na simba atakula majani makavu kama maksai.

8Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka, naye mtoto mdogo ataweka mkono wake kwenye kiota cha fira.

9Hawatadhuru wala kuharibu juu ya mlima wangu mtakatifu wote, kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana kama maji yajazavyo bahari.

10Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu.

11Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.

12Atainua bendera kwa mataifa na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni; atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika kutoka pembe nne za dunia.

13Wivu wa Efraimu utatoweka, na adui wa Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamwonea Yuda wivu, wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.

14Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti hadi upande wa magharibi, kwa pamoja watawateka watu nyara hadi upande wa mashariki. Watawapiga Edomu na Moabu, na Waamoni watatawaliwa nao.

15Bwana atakausha ghuba ya bahari ya Misri; kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake juu ya Mto Frati. Ataugawanya katika vijito saba ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.

16Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake wale waliosalia kutoka Ashuru, kama ilivyokuwa kwa Israeli walipopanda kutoka Misri.

chanzo: Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

WEBREATH · 11:11

«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath