Ukristo
nyuma

Kumbukumbu La Torati 34

1Kisha Mose akaupanda mlima Nebo kutoka tambarare za Moabu mpaka kilele cha Pisga, ngʼambo ya Yeriko. Huko Bwana akamwonyesha nchi yote: kutoka Gileadi mpaka Dani,

2Naftali yote, nchi ya Efraimu na Manase, nchi yote ya Yuda mpaka bahari ya magharibi,

3Negebu na nchi yote kuanzia Bonde la Yeriko, Mji wa Mitende, hadi Soari.

4Kisha Bwana akamwambia, “Hii ndiyo nchi niliyomwahidi Abrahamu na Isaki na Yakobo kwa kiapo niliposema, ‘Nitawapa wazao wako.’ Nimekuruhusu uione kwa macho yako, lakini hutavuka kuingia.”

5Naye Mose mtumishi wa Bwana akafa huko Moabu, kama Bwana alivyokuwa amesema.

6Mungu akamzika huko Moabu, katika bonde mkabala na Beth-Peori, lakini hakuna ajuaye kaburi lake lilipo mpaka leo.

7Mose alikuwa na umri wa miaka mia moja na ishirini alipofariki; hata hivyo nguvu ya macho yake haikufifia wala mwili wake haukudhoofika.

8Waisraeli wakaomboleza kwa ajili ya Mose kwenye tambarare za Moabu kwa siku thelathini, mpaka wakati wa kulia na kuomboleza ulipopita.

9Basi Yoshua mwana wa Nuni alijazwa roho ya hekima kwa sababu Mose alikuwa ameweka mikono yake juu yake. Kwa hiyo Waisraeli wakamsikiliza na wakafanya yale ambayo Bwana alikuwa amemwagiza Mose.

10Tangu wakati huo, katika Israeli hajainuka nabii mwingine kama Mose, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso,

11aliyetenda ishara zote zile za miujiza na maajabu ambayo Bwana alimtuma kuyatenda huko Misri, yaani kwa Farao na maafisa wake wote na nchi yake yote.

12Kwa kuwa hakuna mtu yeyote aliyewahi kuonyesha nguvu nyingi ama kutenda matendo ya kutisha ambayo Mose aliwahi kuyafanya mbele ya Israeli yote.

chanzo: Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

WEBREATH · 11:11

«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25

Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.

WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath