Amosi 6
1Ole wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni, na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria, ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine, ambao watu wa Israeli wanawategemea!
2Nendeni Kalne mkaone kutoka huko; mwende hadi Hamathi iliyo kuu, kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti. Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili? Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?
3Mnaiweka mbali siku iliyo mbaya na kuleta karibu utawala wa kuogofya.
4Ninyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu, na kujinyoosha juu ya viti vya fahari. Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri na ndama walionenepeshwa.
5Ninyi mnapiga vinubi kama Daudi, huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.
6Mnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa, na mnajipaka mafuta mazuri, lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yosefu.
7Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni; karamu zenu na kustarehe kutakoma.
8Bwana Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema: “Nachukia kiburi cha Yakobo, nachukia ngome zake; nitautoa mji wao na kila kitu kilichomo ndani mwake.”
9Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa.
10Kama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina la Bwana.”
11Kwa kuwa Bwana ameamuru, naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.
12Je, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali? Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai? Lakini mmegeuza haki kuwa sumu na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:
13ninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?”
14Maana Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema, “Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli, nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bonde la Araba.”
WEBREATH · 11:11
«He himself gives everyone life and breath and everything else» — Acts 17:25
Breath is one for all: everyone lives by it, whoever they are and whatever they believe. Every day at 11:11 local time people stop for sixty seconds, breathe, and thank GOD for the breath — each in their own words, each within themselves. In that minute we are One Breath.
WEBREATH — the Minute at 11:11, your own local time — we are One Breath